
Umoja wa Mataifa umetangaza kwamba makundi yanayopigana nchini Sudan yanafaidika kutokana na udhibiti wa rasilimali za nchi hiyo, wakati uchumi wa vita ukichangia katika kuendeleza mzozo huo.
Kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ili kufadhili gharama zinazoongezeka za shughuli za kijeshi, pande zinazopigana zinategemea kudhibiti na kutumia vibaya ardhi, njia za biashara na bidhaa, suala ambalo lichangia katika mzozo ambao “unazidi kuwa mrefu.”
Kamisheni hiyo ya Umoja wa Mataifa imetoa wito kwa pande zinazopigana na makampuni yanayofanya kazi katika mnyororo wa usambazaji wa bidhaa nchini Sudan kuhakikisha kwamba zinafuata sheria za kimataifa.
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema: “Utajiri mkubwa wa maliasili wa Sudan unapaswa kuwanufaisha watu wake.”
“Kwa masikitiko, tunachoshuhudia leo si hivyo hata kidogo. Utajiri huo unachangia kudhoofisha haki za binadamu, kuchochea migogoro na kusababisha maumivu na mateso kwa kiwango kikubwa. Uchumi huo wa vita lazima uvunjwe, na jamii ya kimataifa lazima itilie manani zaidi bidhaa na njia za biashara zinazochangia kuendelea kwake,” amesema Volker Türk.
Inafaa kukumbusha kwamba vita kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa kundi la Rapid Support Forces vilizuka Aprili 2023, na hadi sasa vimesababishamauaji ya watu 200,000 na kulazimisha wengine zaidi ya milioni 11 kuwa wakimbizi. Maeneo mengi ya Sudan pia yamekumbwa na njaa kutokana na vita hivyo.