
Mwanza. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amemteua Padri wa Jimbo Katoliki la Geita, Profesa Emmanuel Wabanhu kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT).
Pisa ambaye pia ni Kansela wa chuo hicho na Askofu wa Jimbo Katoliki Lindi amesema uteuzi huo utaanza Agosti Mosi, 2026.
Uteuzi huo umetangazwa jana Jumatano, Julai 15, 2026 kupitia taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha SAUT yenye makao makuu yake jijini Mwanza.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa Profesa Wabanhu anarithi nafasi ya Profesa Juvenalis Asantemungu ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya Makamu Mkuu wa chuo hicho kuanzia Juni 16, 2025 kufuatia changamoto za kiafya na baadaye kifo cha aliyekuwa Makamu Mkuu, Profesa Costa Mahalu.
Profesa Mahalu ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia alifariki dunia Machi 9, 2026 akiwa na umri wa miaka 77.
Msomi huyo mahiri wa sheria na mwanadiplomasia mkongwe alifariki dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia masharti ya Hati ya Chuo Kikuu SAUT ya mwaka 2012 pamoja na marekebisho yake yaliyotolewa kupitia Tangazo la Serikali namba 580 la mwaka 2020 chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu.
Profesa Wabanhu ni Padri wa Jimbo Katoliki Geita na ni Profesa Mshiriki mwenye uzoefu katika taaluma ya teolojia ya maadili akibobea katika maadili tetezi, msomi na mwalimu anayejulikana kwa mchango wake katika taaluma hiyo.
Aliwahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Afrika Mashariki (CUEA) Nairobi nchini Kenya kwa zaidi ya miaka 13 na baadaye alihudumu kwa miaka miwili kwenye wadhifa wa Naibu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia utawala na fedha katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo cha Tabora (AMUCTA), Tanzania.
Katika mchango wake wa kitaaluma, Profesa Wabanhu ameandika vitabu vitano na kuchapisha zaidi ya makala 20 za kitaaluma katika majarida yanayotambuliwa kimataifa.
Ana Shahada ya kwanza ya teolojia kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana (Pontificia Università Urbaniana), Roma nchini Italia, Shahada ya Uzamili ya masomo ya dini, Shahada ya Uzamili ya teolojia, Shahada ya Uzamivu wa Teolojia Takatifu (STD) pamoja na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika maadili ya jamii (biashara) kutoka Chuo Kikuu cha Katholieke Universiteit Leuven, Ubelgiji.
Chuo cha SAUT kimempongeza kwa uteuzi huo na kueleza imani yake kuwa ataongoza vyema taasisi hiyo, huku kikitoa wito kwa wadau wote kumpa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake mapya.