Kigoma. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Kigoma, leo Alhamisi, Julai 16, 2026, itatoa uamuzi wa awali katika kesi ya uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini, iwapo walalamikiwa wana kesi ya kujibu ama la, huku walalamikaji wakiipinga kwa madai kuwa haina mamlaka ya kutoa uamuzi wa namna hiyo.

Uamuzi huo umepangwa kutolewa leo na Jaji Victoria Nongwa, anayesikiliza kesi hiyo, baada ya walalamikaji kufunga kesi upande wao Julai 10, 2026.

Hata hivyo, kabla ya uamuzi huo, walalamikaji wameibuka na hoja mpya wakipinga utaratibu wa Mahakama kuamua kama walalamikiwa wana kesi ya kujibu ili wajitetee au la, huku wakidai kuwa baada ya kufunga ushahidi wao, walalamikiwa walipaswa kuwasilisha utetezi wao moja kwa moja.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya mwaka 2025, inayotokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, imefunguliwa na wananchi wanne wanaojitambulisha kama wapiga kura wa jimbo hilo, Johary Kabourou, Luma Akilimali, Pendo Kombolela na Lumu Mwitu.

Wapiga kura hao wanampinga mbunge wa Jimbo hilo (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo dhidi ya mpinzani wake mkuu, mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo.

Mbali na Baba Levo, ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo, walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini (mlalamikiwa wa kwanza) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mlalamikiwa wa tatu.

Walalamikaji hao wanadai uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi, vikiwemo vitendo vya rushwa na matumizi ya udini vilivyofanywa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Katika kuthibitisha madai yao, walalamikaji hao waliwaita jumla ya mashahidi 16, wakiwemo wao wenyewe, ambao kwa sehemu kubwa ushahidi wao ulitawaliwa na tuhuma za rushwa dhidi ya Baba Levo, kutekwa kwa mashahidi na matumizi ya udini.

Mashahidi hao ndio waliokidhi vigezo vya kutoa ushahidi katika kesi hiyo, yaani wale ambao maelezo yao ya ushahidi wa maandishi yalishawasilishwa mahakamani kabla ya kupanda kizimbani, kama Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za mwaka 2025 zinavyoelekeza.

Mbali na ushahidi wao wa maandishi na wa mdomo wakati wakihojiwa na mawakili wa walalamikiwa kwa maswali ya dodoso, mashahidi hao pia waliwasilisha vielelezo mbalimbali vya nyaraka ngumu na vya kielektroni, hususan picha jongefu (video).

Video hizo zinalenga kuithibitishia Mahakama madai na tuhuma zao dhidi ya mbunge huyo.

Julai 10, 2026, baada ya kumaliza kuwaita mashahidi wao waliokuwa wamekidhi vigezo, walalamikaji waliiomba Mahakama kuwaongezea muda wa kuwasilisha maelezo ya shahidi wa nyongeza, ambaye walidai ni muhimu katika kesi hiyo, Zitto, aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo.

Hata hivyo, maombi hayo yalipingwa vikali na mawakili wa Serikali kwa hoja ambazo ziliungwa mkono na wakili wa Baba Levo.

Mahakama, katika uamuzi wake, ilikubaliana na hoja za walalamikiwa na kuyakataa maombi hayo, pamoja na mambo mengine ikisema kuwa hayakukidhi matakwa ya kanuni za mashauri ya uchaguzi wa wabunge.

Kutokana na uamuzi huo, walalamikaji kupitia wakili wao, John Seka, walilazimika kufunga ushahidi wao.

Baada ya hatua hiyo, Jaji Nongwa alielekeza mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja zao za maandishi kuhusu iwapo walalamikiwa wana kesi ya kujibu ama la ndani ya siku tatu, huku akipanga kutoa uamuzi wa suala hilo leo Alhamisi.

Uamuzi huo ndio utakaotoa hatima ya kesi hiyo kuendelea au kufa kifo cha kawaida.

Kama Mahakama itaamua walalamikiwa wana kesi ya kujibu, watalazimika kuwasilisha utetezi wao dhidi ya madai na tuhuma zilizoibuliwa na walalamikaji.

Iwapo Mahakama itaamua walalamikiwa hawana kesi ya kujibu, basi kesi hiyo itaishia hapo.

Hata hivyo, walalamikaji katika hoja zao hizo, ambazo Mwananchi limeziona, wamepinga utaratibu uliotolewa na Mahakama wa kutoa uamuzi kama walalamikiwa wana kesi ya kujibu ama la.

Katika hoja zao, pamoja na mambo mengine, wanadai Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa uamuzi huo kwa kuwa utaratibu huo haupo kisheria.

Wanadai mashauri ya uchaguzi ni mashauri maalumu yanayoendeshwa kwa mujibu wa Katiba, sheria na kanuni, na kwamba si Katiba wala Sheria ya Uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais ya mwaka 2024, wala Kanuni za Mashauri hayo za mwaka 2025, zinazotoa utaratibu huo.

Badala yake, wamedai kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo na kanuni hizo, baada ya walalamikaji kufunga ushahidi wao, hatua inayofuata ni walalamikiwa kuwasilisha ushahidi wa utetezi wao ndani ya saa 48.

Wanadai hatua ya Mahakama kutoa utaratibu huo ambao haupo kwenye sheria mahsusi ni sawa na kutunga sheria mpya, jambo ambalo Mahakama haina mamlaka nalo, kwani wajibu wake ni kutafsiri sheria.

Hivyo, wanaiomba Mahakama iamue kuwa ilijielekeza vibaya kwa kutoa utaratibu huo.

Hata hivyo, wanadai kuwa kama Mahakama itafikia hitimisho kuwa utaratibu huo ni sahihi, basi ushahidi wao umeibua hoja ambazo walalamikiwa wanapaswa kujibu kwa kuwasilisha utetezi wao.

Kabla ya kuanza usikilizaji wa kesi hiyo kwa kupokea ushahidi wa walalamikaji, Mahakama, kwa kushauriana na mawakili wa pande zote, iliunda viini saba vya msingi wa uamuzi, ambavyo ni hoja zinazobishaniwa na zitakazoiongoza Mahakama kufikia hitimisho la uamuzi wake.

Hoja hizo, ambazo ndizo ushahidi wa walalamikaji ulijikita kuzithibitisha, ni pamoja na iwapo mlalamikiwa wa kwanza, yaani Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo, alikiuka masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais ya mwaka 2024.

Hoja ya pili hadi ya tano zinamhusu mlalamikiwa wa pili, Baba Levo, ambazo ni:

Iwapo alitumia hoja za udini wakati wa kampeni, iwapo alitumia lugha yenye lengo la kuharibu taswira ya mgombea wa ACT-Wazalendo, iwapo yeye, viongozi na watu wake walishiriki katika vitendo vya rushwa wakati wa kampeni vilivyomnufaisha katika uchaguzi huo.

Hoja nyingine inayomhusu Baba Levo ni iwapo yeye, viongozi wa chama chake na watu wake walishiriki katika vitendo haramu (kuwateka mashahidi, kama walivyodai walalamikaji), ambavyo vilimnufaisha katika uchaguzi huo.

Hoja nyingine ni iwapo madai ya walalamikaji yatathibitika, ni kwa kiasi gani yaliathiri matokeo ya uchaguzi huo, na mwisho ni nafuu gani ambazo wadaawa (kila upande) wanastahili.

Katika maelezo ya hoja zao, walalamikaji wamechambua ushahidi unaojibu viini hivyo vya uamuzi kwa kila kiini, kama ulivyowasilishwa na mashahidi mbalimbali.

“Kwa msingi huo, tunawasilisha kwamba ushahidi uliopo mbele ya Mahakama umevuka kiwango cha chini kinachohitajika na sheria katika hatua hii. Hoja zote zinazohitaji majibu kutoka kwa walalamikiwa zimeibuliwa wazi kupitia ushahidi uliowasilishwa na walalamikaji,” amesema Wakili Seka na kusisitiza:

“Kwa hiyo, njia pekee inayoendana na sheria, haki na mwenendo sahihi wa mashauri ni kuwataka walalamikiwa kuingia katika utetezi wao ili Mahakama ipate fursa ya kutathmini ushahidi wote kabla ya kutoa uamuzi wa mwisho.”

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kitakachoamuliwa baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *