
Dalili za kuongezeka kwa mvutano kati ya Eritrea na Ethiopia zimeibua wasiwasi wa uwezekano wa kurejea mgogoro kati ya mataifa hayo mawili ya Pembe ya Afrika.
Serikali ya Eritrea imeendelea kusisitiza utayari wake wa kulinda mamlaka na mipaka ya nchi dhidi ya kile inachokieleza kuwa ni ya kujitanua ya Ethiopia, huku ikionya kuwa haitakubali hatua yoyote itakayohatarisha uhuru na usalama wa taifa hilo.
Mvutano huo umeibua hofu ya kurejea kwa mapigano katika eneo la Pembe ya Afrika, ambalo limekuwa likikabiliwa na changamoto za usalama na migogoro ya kisiasa katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa upande mwingine, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa tofauti zinazohusu maslahi ya kimkakati na upatikanaji wa njia za baharini zinaweza kuzidisha mvutano kati ya nchi hizo mbili iwapo hazitapatiwa suluhu kupitia mazungumzo ya kidiplomasia.
Ripoti ya Shirika la Habari la IRNA, ikinukuu tovuti ya Africa Live, imeeleza kuwa mvutano wa sasa kati ya Ethiopia na Eritrea una uwezo mkubwa wa kuyumbisha usalama wa eneo zima la Pembe ya Afrika, huku mabadiliko ya msimamo wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, yakizua wasiwasi kutokana na kauli zake za kimakabiliano.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Abiy Ahmed, ambaye mwaka 2019 alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kutokana na juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa amani na Eritrea, sasa ameanza kuchukua msimamo mkali. Anadai kuwa Eritrea imekuwa changamoto kuu kwa serikali zote za Ethiopia tangu enzi za Mfalme Haile Selassie, aliyeiongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1930 hadi 1974.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa Eritrea kwa muda mrefu imekuwa ikipinga kile inachokiona kuwa ni madai ya Ethiopia ya kutaka kuitawala. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wakati makoloni ya zamani ya Italia kama Somalia na Libya yalipopata uhuru, Eritrea haikupata fursa hiyo, bali iliunganishwa na Ethiopia.