Dalili za ukomo wa hedhi

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 7

Miezi michache iliyopita, nilichapisha ujumbe kwenye LinkedIn kuhusu ukungu wa ubongo (brain fog). Niliuandika kwa haraka ndani ya dakika 10, nikielezea jinsi nilivyolazimika, kwa mara ya kwanza katika miaka yangu 20 ya kazi, kutumia madokezo nilipokuwa nikisoma habari mubashara kutokana na ukungu wa ubongo uliosababishwa na kipindi cha kabla ya ukomo wa hedhi (perimenopause).

Sikutarajia ujumbe huo kupata mwitikio mkubwa kiasi hicho.

Cha kushangaza, mada hiyo ilizua mjadala mpana na nikapokea wimbi kubwa la huruma na uungwaji mkono. Kulikuwa na karibu maoni 400 kwenye LinkedIn, ujumbe kadhaa wa faragha, pamoja na mamia ya maoni zaidi chini ya makala ya BBC kuhusu suala hilo. Maoni mengi yalikuwa na ujumbe unaofanana: watu waliniita “jasiri” kwa kuzungumzia jambo hilo hadharani au walinisifu kwa “kufanya ukungu wa ubongo uonekane kuwa jambo la kawaida.”

Wakati huo sikujihisi kuwa jasiri (wala wa kawaida), lakini hali hiyo ilinifanya nitambue jinsi baadhi ya dalili za kipindi cha kabla ya ukomo wa hedhi na ukomo wa hedhi zilivyozungukwa na unyanyapaa wa kijamii na hisia za aibu, licha ya kwamba hali hizi huathiri karibu nusu ya watu duniani katika kipindi fulani cha maisha yao.

Nyota wa Hollywood kama Oprah Winfrey na Halle Berry, pamoja na watangazaji wa televisheni, wamezungumza hadharani kuhusu uzoefu wao binafsi wa ukomo wa hedhi na athari zake. Vivyo hivyo, Gwyneth Paltrow mwaka 2018 alitoa wito wa “kutafakari upya mtazamo wa kijamii kuhusu ukomo wa hedhi.”

Kumekuwa pia na mabadiliko katika eneo hili. Kwa mfano, kuanzia mwaka huu, uchunguzi wa ukomo wa hedhi (menopause screening) utaongezwa rasmi katika vipimo vya kawaida vya afya nchini Uingereza kwa wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 40.

Utafiti uliohusisha takribani wanawake 1,600, uliochapishwa mwezi Oktoba na Chuo Kikuu cha London (UCL), uligundua kuwa zaidi ya asilimia 75 ya washiriki walihisi hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu ukomo wa hedhi.

Matokeo hayo yanaashiria kuwepo kwa pengo kubwa la maarifa kuhusu suala hilo.

Gwyneth Paltrow

Chanzo cha picha, Getty Images for BAFTA

Aidha, wanawake wengi wanasema kuwa kuzungumzia ukomo wa hedhi bado kunachukuliwa kuwa mwiko katika jamii, jambo linalowafanya wahisi kushindwa kulizungumzia kwa uwazi.

Mwanamke mmoja mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, ambaye ni profesa wa chuo kikuu na mtaalamu wa sera za jamii, aliniambia kupitia ujumbe kwamba amejifunza kufanya mzaha na kucheka kuhusu “nyakati zake za ukomo wa hedhi” akiwa na wenzake wanawake kazini.

Hata hivyo, aliongeza kuwa hali hiyo bado “inaaibisha,” hasa anaposahau baadhi ya istilahi za kitaaluma katika fani yake.

Lakini kuficha au kujitahidi kuficha dalili za ukomo wa hedhi kunaweza kuwa jambo linalochosha sana kihisia na kimwili.

Dkt. Finola Barton, daktari wa familia na mtaalamu kutoka British Menopause Society, anasema:

“Nguvu zinazotumika kujifanya kuwa kila kitu kiko sawa au kufidia changamoto ambazo wanawake hukumbana nazo mara nyingi huwapunguzia akiba yao ya nguvu, na kuwafanya wafikie hatua ya kuchoka na kuhisi kushindwa mapema zaidi wanapokabiliwa na shinikizo.”

Kwa maoni yake, hali hiyo inaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa hatari ya uchovu wa kupindukia kazini , na pia kuibua swali la iwapo kitendo chenyewe cha kuficha na kutosema wazi kuhusu dalili za ukomo wa hedhi kinaathiri maisha ya wanawake kwa njia hasi.

Kuficha dalili za ukomo wa hedhi na hatari ya uchovu wa kiakili

NHS ina orodha ya dalili 34 zinazoweza kuhusishwa na ukomo wa hedhi, ambazo baadhi yake ni za kawaida zaidi kuliko nyingine. Nyingi ya dalili hizi zinaweza kuwa kali na kuathiri maisha ya kila siku.

Mwanamke mmoja aliyewasiliana nami baada ya kusoma chapisho langu la LinkedIn alieleza kuwa kupungua kwa kiwango cha vichocheo vya estrojeni kulimsababishia ukavu wa uke, tatizo lililofanya hata kutembea kuwa jambo lenye maumivu na ugumu.

Rafiki yangu mmoja aliniambia kuwa ana tatizo la kibofu dhaifu. Alisema tatizo hilo lilianza ghafla kana kwamba “lilitokea usiku mmoja,” na wakati mwingine hushindwa kufika chooni kwa wakati.

Alisema mwenyewe, “Tatizo hili linanisumbua kuliko kitu kingine chochote,” ndiyo maana hayuko tayari tena kurudi kufanya kazi ofisini na anapendelea kufanya kazi akiwa nyumbani.

Mwanamke mwingine aliniambia kuwa huepuka kuhudhuria mikusanyiko ya kijamii kwa sababu anapopata ukungu mkali, hushindwa kufuatilia vizuri mazungumzo.

Watu wengine wengi walishiriki mbinu zao za kukabiliana na hali hiyo. Baadhi yao huweka feni kwenye madawati yao ili kupunguza joto la ghafla (hot flashes), huku wengine, kama mimi, wakichukua maelezo kila mara ili wasipoteze mwelekeo wa mawazo wakati wa mikutano na mawasilisho kutokana na ukungu wa ubongo.

Kuficha dalili au kujifanya kwamba ukomo wa hedhi (menopause) ni jambo la kawaida lisilohitaji kuzungumziwa hufanya kipindi hiki kuwa kigumu zaidi na chenye mateso makubwa.

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images

Kwa upande mmoja, juhudi hizi zinaonesha ubunifu na uthabiti wa wanawake ambao, licha ya dalili zinazoweza kuwa kali sana, bado hupata njia ya kukabiliana na hali hiyo na kuendelea na maisha yao.

Fiona Clark, mwandishi wa kitabu The Battles of Menopause, anaamini kwamba wanawake wengi hupitia hatua mbalimbali baada ya kuanza kupata dalili za ukomo wa hedhi. Anasema: “Kwanza hupitia kipindi cha kuchanganyikiwa na kukataa hali hiyo, kisha hupitia kipindi cha huzuni, na hatimaye hufikia hatua ya kuikubali.”

Lakini anasisitiza: “Unapoficha au kufunika hali hiyo, unaacha kutafuta matibabu na msaada unaouhitaji.”

Kuficha dalili za ukomo wa hedhi mahali pa kazi kunaweza kuwa changamoto kubwa. Kulingana na ripoti ya serikali ya mwaka 2024, takribani wanawake milioni nne nchini Uingereza wenye umri wa kati ya miaka 45 na 55 wako kazini, umri ambao wengi hupitia kipindi cha ukomo wa hedhi.

Joe Brewis, profesa wa usimamizi wa rasilimali watu katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Huria (Open University Business School) nchini Uingereza, anasema kuwa watu wanapoficha dalili zao mahali pa kazi, hali hiyo inaweza kuwa na gharama zisizoonekana, gharama ambazo wachumi huziona kama kupungua kwa ubora wa kazi na uzalishaji.

Anasema, “Kwa maneno mengine, nguvu na nishati ambazo mtu hutumia kuficha hali yake humletea mzigo wa ziada wa kisaikolojia na kimwili.”

Baadhi ya wanawake hata hulazimika kuacha kazi zao. Kulingana na ripoti ya mwaka 2022 ya Fast Company, iliyotokana na utafiti uliowahusisha wanawake 4,000 nchini Uingereza, inakadiriwa kuwa mwanamke mmoja kati ya 10 wenye umri wa miaka 40 hadi 55 anayefanya kazi amelazimika kuacha ajira kutokana na dalili kali za ukomo wa hedhi.

Nyota wa Hollywood, akiwemo Halle Berry, wamezungumza hadharani kuhusu uzoefu wao binafsi wa kukabiliana na ukomo wa hedhi (menopause) na jinsi ulivyoathiri maisha yao.

Chanzo cha picha, FilmMagic via Getty Images

Kulingana na Joe Brewis, “Shinikizo hili linaweza kuwafanya wanawake wajitenge au kujipunguza thamani yao wenyewe, kwa mfano kwa kutotuma maombi ya kupandishwa cheo au hata kukubali nafasi ya chini yenye mshahara mdogo ili waweze kukabiliana na hali hiyo.”

Anaongeza kuwa: “Watu wanaweza kujitahidi zaidi ili kuepuka kuonekana kana kwamba utendaji wao umeshuka au hawafanyi kazi ipasavyo. Kwa mfano, wanapokuwa na dalili za kawaida kama vile kupungua kwa uwezo wa kuzingatia au uchovu, wanaweza kufanya kazi kwa saa nyingi zaidi ili kuhakikisha wamekagua kazi yao mara ya pili na kwamba hakuna makosa yaliyosalia bila kugunduliwa.”

Wanawake wa Japani na ukomo wa hedhi

Bila shaka, hatupaswi kusahau kwamba ukomo wa hedhi si uzoefu unaofanana kwa kila mwanamke, wala si jambo hasi kwa kila mtu. Baadhi ya wanawake huliona kipindi hiki kwa mtazamo chanya, hivyo ni muhimu kuepuka kufanya ujumlishaji kuhusu uzoefu wa wanawake wote.

Katika utamaduni wa Japani, kipindi hiki wakati mwingine huitwa “masika ya pili” (second spring), neno linaloashiria mpito wenye matumaini kuelekea msimu mpya wa maisha.

Dkt. Megan Arnott, mwanaanthropolojia wa mageuzi katika Chuo Kikuu London, anasema:

“Katika nchi nyingi bado kuna aina fulani ya mwiko au mtazamo hasi kuhusu ukomo wa hedhi, ingawa inaonekana kwamba mitazamo hiyo inaanza kubadilika katika miaka ya hivi karibuni.”

Pia anaelekeza kwenye tamaduni na nchi ambazo zimeanza kuutazama ukomo wa hedhi kwa njia chanya zaidi.

“Katika jamii nyingi za asili, zikiwemo za Wamarekani wa Asili na Wamaya, ukomo wa hedhi huonekana kama hatua ya mpito kuelekea kipindi cha hekima na uongozi, ambapo wanawake hupata heshima kubwa zaidi na ushawishi mpana zaidi.

m

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa sasa, ukomo wa hedhi umekuwa sekta yenye faida kubwa kibiashara. Kuanzia virutubisho vya lishe, programu za kufuatilia dalili, vifaa vya tiba vinavyovaliwa kichwani, hadi wakufunzi wa mtindo wa maisha, wengi wanatoa bidhaa na huduma zinazolenga wanawake wanaopitia kipindi hiki.

Mitandao yangu ya kijamii imejaa matangazo ya tiba za asili zinazodai kusaidia wanawake wa umri wa makamo.

Thamani ya soko la bidhaa zinazohusiana na ukomo wa hedhi ilikadiriwa kuzidi dola bilioni 17 mwaka 2024, na inatarajiwa kufikia zaidi ya dola bilioni 24 ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba mara nyingi hakuna suluhisho moja linalotosha peke yake.

Bi Brewis anasisitiza kuwa mahali pa kazi, waajiri wanapaswa kuwa waangalifu na wenye busara katika namna wanavyowaunga mkono wafanyakazi wanaopitia ukomo wa hedhi.

Anaamini kwamba wasimamizi wanapaswa kupatiwa mafunzo ya jinsi ya kufanya mazungumzo nyeti kuhusu suala hilo na kurekebisha mazingira ya kazi kulingana na mahitaji ya kila mfanyakazi. Pia anaongeza kuwa ni muhimu sana ukomo wa hedhi utambuliwe rasmi kama sababu halali ya kupewa likizo.

“Baadhi ya watu hawataki kabisa kuzungumzia ukomo wao wa hedhi mahali pa kazi, hata kama mwajiri wao anaunga mkono na kujali wafanyakazi wake; hiyo ni haki yao. Lakini hatua madhubuti zinaweza, na zinapaswa, kuanzisha mazungumzo kuhusu suala hili na kupunguza mzigo wa unyanyapaa unaolizunguka.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *