DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Salum Waziri, amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta ya viwanda biashara hususani katika Kongani ya Viwanda ya Kwala inayotarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo makubwa ya viwanda Afrika.
Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi ya biashara ikiwemo kukamilisha miundombinu muhimu ya gesi, Reli ya Kisasa (SGR) na barabara ili kuongeza ufanisi wa uwekezaji na usafirishaji katika eneo hilo na itaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazijitokeza viwandani.

Balozi Waziri ametoa kauli hiyo Julai 16, 2026 wakati wa ziara yake katika Kiwanda cha King Lion na Kongani ya Viwanda ya Kwala mkoani Pwani kwa lengo la kujionea shughuli za uzalishaji na kusikiliza na kutatua changamoto zinazojitokeza katika viwanda hivyo.
Aidha, ameongeza kuwa uwekezaji mkubwa uliopo katika viwanda hivyo inaonesha dhamira ya Tanzania ya kujenga uchumi wa viwanda na mazingira mazuri na rafiki ya biashara yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya Kibaha, Nickson John amesema Kongani ya Kwala inatarajiwa kuwa kitovu kikubwa cha viwanda nchini, ambapo mradi huo ukikamilika utakuwa na viwanda 250 na kuzalisha ajira zaidi ya 50,000 kwa vijana pamoja na kuongeza mapato ya halmashauri.