ARUSHA: Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Delilah Kimambo, amesema kuwa wagonjwa 9,507 tayari wamepata huduma za matibabu bure kupitia kambi ya madaktari bingwa na wabobezi inayoendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kutembelea hospitali za rufaa za serikali na binafsi zinazoshiriki kutoa huduma katika kambi hiyo, Dk. Kimambo alisema lengo la huduma hizo ni kuwafikia wananchi, hasa wenye kipato cha chini, na kuwapatia matibabu bora bila malipo.

Alisema kambi hiyo, ambayo huhudumia zaidi ya wagonjwa 3,500 kwa siku, inatoa huduma mbalimbali za afya ikiwemo matibabu ya dharura, uchunguzi wa magonjwa, upasuaji mdogo na mkubwa pamoja na huduma za macho.
Kwa mujibu wa Dk. Kimambo, zaidi ya miwani 10,000 tayari imetolewa kwa wagonjwa wenye matatizo ya macho, huku wastani wa wagonjwa 47 wakifanyiwa upasuaji mdogo wa macho kila siku.
Alisema kambi hiyo imeandaliwa na kuratibiwa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, ambaye pia ni Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, kwa baraka za Rais Samia Suluhu Hassan.
“Uwepo wa kambi hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa Arusha, hasa wenye kipato cha chini. Wananchi wanapaswa kumpongeza Mbunge wao kwa kuwaletea huduma muhimu za afya karibu nao,” alisema Dk. Kimambo.

Aidha, aliwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kupima saratani ya matiti na saratani ya shingo ya kizazi, akieleza kuwa magonjwa hayo mara nyingi huanza bila dalili, hivyo uchunguzi wa mapema ni muhimu katika kuokoa maisha.
“Haya magonjwa huweza kuanza bila dalili zozote. Ni muhimu wanawake wakajitokeze kupima afya zao mara kwa mara ili kujikinga na madhara makubwa yanayoweza kujitokeza baadaye,” alisema.
Akizungumzia magonjwa yasiyoambukiza, Dk. Kimambo alisema watu zaidi ya 2,500 tayari wamepimwa na kupatiwa matibabu, akisisitiza kuwa huduma zote muhimu zinapatikana kupitia madaktari bingwa na wabobezi waliopo kambini.

Aliongeza kuwa hospitali zote zilizo chini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili zinashiriki katika kambi hiyo na zinaendelea kutoa huduma, ikiwemo upasuaji mkubwa na mdogo, hadi nyakati za usiku.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Charles Mkombachepa, alisema ujio wa gari la kisasa la Hospitali ya Taifa Muhimbili lenye uwezo wa kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo upasuaji, umeongeza ubora wa huduma zinazotolewa kambini.
Alisema mafanikio ya kambi hiyo yanaonesha ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Afya, taasisi za afya za umma na binafsi pamoja na wadau wengine.
Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Paul Makonda, alisema hiyo ni mara ya tatu kwa kambi hiyo kufanyika mkoani Arusha mara mbili akiwa Mkuu wa Mkoa na sasa akiwa Mbunge. Alisisitiza kuwa kambi hiyo itakuwa ikifanyika kila mwaka ili kuwasaidia wananchi kupata huduma bora za afya na kuchangia ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya uchumi.