
Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi waliotembelea Kijiji cha Bima katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, wamepongeza uwepo wa jukwaa hilo na kuomba liendelee kuandaliwa kila mwaka.
Wananchi hao pia wameiomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira) kushirikisha kampuni nyingi zaidi za bima katika maonyesho yajayo ili wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kupata elimu na huduma za bima katika eneo moja.
Mwaka huu, Kijiji cha Bima kilivutia takribani kampuni 40 za bima zilizopata nafasi ya kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali za bima, kujipatia wateja wapya pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wateja wao.
Akizungumza wakati wa kumalizika maonyesho hayo, Anita Ndimbo, mmoja wa wananchi waliotembelea Kijiji hicho, amesema utaratibu huo umeleta urahisi mkubwa kwa wananchi kufikia kampuni nyingi za bima kwa wakati mmoja na kufanya uamuzi sahihi kuhusu huduma wanazohitaji.
“Huu ni utaratibu mzuri sana kwani imekuwa rahisi kufikia kampuni nyingi kwa wakati mmoja na kufanya uamuzi sahihi. Tira ina wajibu wa kufikia kampuni nyingi zaidi za bima ziwe sehemu ya utaratibu huu, huku wananchi wakihamasishwa zaidi kuhusu umuhimu wa bima,” amesema.
Kwa upande wake, Mgeni Ali amesema alifurahishwa na uwepo wa Kijiji cha Bima kwa kuwa kilimpa fursa ya kupata elimu kuhusu huduma mbalimbali za bima ambazo hapo awali hakuwa akizifahamu.
“Nilikuja Sabasaba kujionea mambo mbalimbali, lakini nilipoona kuna Kijiji cha Bima nilivutiwa kuja kupata elimu. Kuna aina nyingi za bima ambazo sikuwa nazifahamu. Sasa nina uelewa wa kutosha wa kufanya maamuzi sahihi,” amesema.
Naye Suleiman Mohamed amewataka wananchi kuondokana na dhana potofu kwamba bima ni kwa ajili ya afya pekee, akieleza kuwa zipo huduma nyingi za bima zinazolenga kulinda maisha na mali za wananchi.
“Kupitia kijiji hiki cha bima nimejifunza mambo mengi. Awali,niliona umuhimu wa bima ya afya tu, lakini sasa nimefahamu kuwa zipo pia bima za mifugo, nyumba, biashara na nyingine nyingi,” amesema.
Kijiji cha bima ni jukwaa la kila mwaka linaloratibiwa na Tira kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya bima kwa lengo la kuwasogezea wananchi elimu ya bima, ushauri wa kitaalamu pamoja na huduma mbalimbali za bima katika eneo moja.
Kupitia jukwaa hilo, wananchi hupata nafasi ya kujifunza umuhimu wa kuwa na bima mbalimbali zinazolinda maisha, afya, mali, biashara na uwekezaji wao dhidi ya vihatarishi vinavyoweza kujitokeza.
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi Kijiji cha Bima baada ya kumalizika kwa Maonyesho ya Sabasaba, Mkurugenzi wa Tafiti na Uendelezaji wa Soko wa Tira, Zakaria Muyengi amezipongeza kampuni za bima kwa mchango wao katika kufanikisha shughuli hiyo.
Amesema kupitia Kijiji cha Bima wananchi wengi wamepata elimu ya bima pamoja na huduma mbalimbali zilizosaidia kutatua changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo.
“Kupitia fursa hii tumeweza kutoa elimu kwa wananchi na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili. Bado tunayo kazi kubwa ya kuendelea kuwaelimisha Watanzania kuhusu masuala ya bima na umuhimu wake,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia huduma za bima kama nyenzo muhimu ya kudhibiti vihatarishi na kujenga ustahimilivu wa kifedha kwa watu binafsi, biashara na taasisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kijiji cha Bima, Kelvin Mushi, amesema mafanikio yaliyopatikana mwaka huu yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya Tira na kampuni mbalimbali za bima.
“Tunaamini mwakani tutafanya vizuri zaidi na kuendelea kuboresha Kijiji cha Bima ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hilo ndilo lengo kuu la kuanzishwa kwa jukwaa hili,” amesema, huku akiipongeza Tira kwa kubuni mpango huo.
Maonyesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (Sabasaba) yalianza Juni 28, 2026 na kuhitimishwa Julai 14, 2026, yakivutia maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali za nchi kila siku.