BAADA ya Mashujaa kutangaza kuachana na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, klabu hiyo inaendelea kufanya mazungumzo na makocha wanne kwa ajili ya mmojawapo kuinoa timu hiyo kwa msimu ujao wa 2026-2027.

Julio aliyeingia kikosini hapo Februari 2026 akichukua nafasi ya Salum Mayanga, amemaliza msimu wa 2025-2026 na kikosi hicho kikishika nafasi ya 11 na pointi 33 katika msimamo wa Ligi Kuu.

Chanzo kimesema kinaheshimu mchango wa kocha Julio, lakini lazima maisha mengine yaendelee, hivyo wanafanya mazungumzo na makocha wengi akiwemo Zuberi Katwila aliyeipandisha Geita Gold, Amani Josiah aliyeisaidia Dodoma Jiji kumaliza nafasi ya tisa na pointi 35 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Wengine ni Fikiri Elias aliyeiongoza Coastal Union ya Tanga kumaliza ikiwa nafasi ya nane na pointi 36 kwenye ligi msimu uliomalizika na Mecky Maxime ambaye aliachana na Mbeya City kabla ya kumalizika kwa msimu.

“Ba do hatujafikia mwafaka, ingawa kwa baadhi yao mazungumzo yana muelekezo mzuri, kama tutafanikisha kumpata mmoja wapo tutaweka wazi,” kimesema chanzo hicho na kuongeza.

“Tunahitaji kupata kocha kwa haraka kwani tayari timu imepiga kambi Kunduchi, Dar es Salaam tangu Julai 15, tunafahamu msimu ujao unaotarajia kuanza Agosti 14 utakuwa mgumu, hivyo lazima kila kitu kiwekwe sawa mapema.”

Chanzo hicho kilifafanua ishu ya kiungo wa timu hiyo, Salum Kihimbwa aliyekuwa anahusishwa na Simba, tayari wameshamuongezea mkataba wa mwaka mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *