IRINGA: Mkoa wa Iringa umeingia katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030 ukiwa na taswira ya mafanikio yanayoonekana kwa macho: mapato ya Serikali yameongezeka, fedha za maendeleo zimeongezeka, na miradi ya afya, elimu, maji na miundombinu inaendelea kubadili maisha ya wananchi.
Taarifa ya utekelezaji wa ilani kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026 inaonyesha mkoa umefanikiwa kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato huku fedha nyingi zikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hatua ambayo viongozi wa chama na Serikali wanasema imeendelea kutoa matokeo chanya katika utoaji wa huduma za kijamii.
Akiwasilisha taarifa hiyo katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa serikali za mitaa na wananchi katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa imekusanya zaidi ya Sh Bilioni 72, ikiendeleza rekodi ya kuvuka malengo kwa miaka mitano mfululizo, huku halmashauri zote za mkoa zikikusanya zaidi ya Sh Bilioni 39 za mapato ya ndani.
Kwa mujibu wa Kheri, ongezeko hilo la mapato limeongeza uwezo wa Serikali kufadhili miradi ya maendeleo, ambapo zaidi ya Sh Bilioni 287 zimeelekezwa katika sekta za afya, elimu, maji, kilimo, barabara na huduma nyingine za msingi.
Katika sekta ya afya, alisema Serikali imeendelea kujenga na kuboresha hospitali, vituo vya afya na zahanati pamoja na kuajiri watumishi wapya 423 wa kada mbalimbali ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo, alikiri kuwa bado mkoa unakabiliwa na upungufu wa zaidi ya watumishi 2,100, hususan wataalamu wa radiolojia, famasia, usingizi na madaktari wa meno.

Sekta ya elimu nayo imeendelea kunufaika kupitia ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, maktaba na nyumba za walimu, huku zaidi ya asilimia 98 ya shule za msingi na shule zote za sekondari za Serikali zikiendelea kutekeleza mpango wa chakula shuleni, hatua inayochangia kuongeza mahudhurio na kuboresha ufaulu wa wanafunzi.
Katika huduma za maji, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) inaendelea kutekeleza miradi 16 yenye thamani ya zaidi ya Sh Bilioni 39 katika wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi, ambapo baadhi tayari zimeanza kuhudumia wananchi na mingine iko katika hatua za mwisho za kukamilika.
Wakati huo huo, miradi ya ujenzi na matengenezo ya barabara kupitia TANROADS na TARURA inaendelea kuboresha mtandao wa usafiri ndani ya mkoa, huku upanuzi wa mkongo wa taifa unaotekelezwa na TTCL ukitarajiwa kuongeza matumizi ya teknolojia na kukuza uchumi wa kidijitali.

Mbali na miundombinu, Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta za kilimo, umwagiliaji, ardhi na uwekezaji kupitia miradi ya kuongeza uzalishaji, utoaji wa hati za ardhi na utatuzi wa migogoro ya ardhi, hatua zinazolenga kuongeza tija ya uzalishaji na kuvutia uwekezaji.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Daudi Yassin, alisema Kamati ya Siasa ya Mkoa ilifanya ziara katika wilaya zote na kujiridhisha kuwa miradi mingi inayotekelezwa chini ya ilani imefikia hatua nzuri na inaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Alitaja baadhi ya miradi iliyokaguliwa kuwa ni shule mpya za sekondari, Chuo cha VETA, mradi wa uzalishaji wa hewa tiba (Medical Oxygen), barabara, miradi wa umwagiliaji na uwanja wa ndege.
Pamoja na pongezi kwa hatua zilizofikiwa, wabunge wa mkoa huo walitoa mapendekezo ya maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika kipindi kijacho.
Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, alisema mafanikio yaliyopatikana yanapaswa kwenda sambamba na kuboresha miundombinu ya lango la kuingilia Mkoa wa Iringa ili liakisi hadhi ya mkoa huo kama kitovu cha utalii na biashara.
Pia alisisitiza umuhimu wa kurejeshwa kwa timu ya ligi kuu mkoani humo ili kuchochea uchumi na maendeleo ya michezo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kalenga, Jackson Kiswaga, aliitaka Serikali kuendelea kushirikiana na wabunge katika kutatua changamoto za wananchi, zikiwemo ukarabati wa shule kongwe, uboreshaji wa barabara za vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na kuongeza watumishi katika sekta za afya na elimu.
Alisema pia kuna umuhimu wa kuongeza elimu kwa wananchi kuhusu fidia, matumizi ya nishati na usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuongeza ushiriki wa jamii katika maendeleo ya mkoa.
Akihitimisha, Kheri James alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuielekezea Iringa fedha za maendeleo, akisema usimamizi madhubuti wa miradi umewezesha sehemu kubwa ya miradi kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma zinazoboresha maisha ya wananchi.
Alisema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Ilani ya CCM ili kuhakikisha uwekezaji unaoendelea unatafsiriwa kuwa huduma bora, fursa za kiuchumi na maendeleo endelevu kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa.