
Serikali ya Misri imeituhumu Ethiopia kuwa imefanya ‘uzembe na haina uwajibikaji” katika usimamizi wa mafuriko ya Mto Nile kupitia uendeshaji wa upande mmoja wa bwawa lake kubwa, ikisema hatua hizo zimeongeza mafuriko nchini Sudan na kutishia moja kwa moja ardhi na maisha ya Wamisri, huku mgogoro wa muda mrefu kuhusu bwawa hilo linalojulikana kama Grand Ethiopian Renaissance Dam (GERD) ukishaidi.
Taarifa ya Wizara ya Rasilimali za Maji na Umwagiliaji ya Misri imesema kuwa suala kuu ni “mafuriko ya Nile na usimamizi wa upande mmoja wa Ethiopia wa bwawa lake kinyume na sheria za kimataifa.”
Wizara hiyo ilieleza Ijumaa kuwa imekuwa ikifuatilia matukio ya mafuriko ya mwaka huu na kuyahusisha moja kwa moja na “hatua za upande mmoja zisizo na uwajibikaji zinazochukuliwa na Ethiopia katika kuendesha bwawa lake haramu, linalokiuka sheria za kimataifa.”
Mamlaka za Misri zimetangaza hatua za tahadhari kukabiliana na kuongezeka kwa kiwango cha maji ya Nile na mafuriko ya ardhi kando ya kingo zake, huku mgogoro ukiendelea baina ya Misri na Sudan kwa upande mmoja, na Ethiopia kwa upande mwingine, kuhusu kujazwa na kuendeshwa kwa bwawa hilo la Ethiopia.
Hatua hiyo ilitangazwa kupitia taarifa za serikali siku moja baada ya Waziri Mkuu wa Misri, Mostafa Madbouly, kutoa onyo kuhusu athari za mafuriko ya Nile.
Katika kikao cha Alhamisi, Madbouly alisema serikali inatarajia viwango vya maji ya Nile kuendelea kuongezeka hadi mwisho wa Oktoba kutokana na msimu wa mvua na mafuriko.
Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty, alisema kuwa “ukosefu wa uratibu kuhusu uendeshaji wa bwawa umepelekea mafuriko makubwa nchini Sudan katika wiki za hivi karibuni,” akisisitiza kuwa “hatua za upande mmoja za Ethiopia kuhusu bwawa hilo ni ukiukaji wa sheria za kimataifa.”
Katika mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Sudan huko Port Sudan, Abdelatty aliongeza kuwa “Misri inahifadhi kikamilifu haki yake, kama inavyodhaminiwa na sheria za kimataifa, kutetea maslahi yake ya msingi na haki zake za maji kwa njia yoyote ile endapo maslahi hayo yatatishiwa au kuathiriwa.”
Serikali ya Ethiopia ilizindua rasmi Bwawa la GERD katika Mto Nile wa Bluu mnamo Septemba 9, baada ya miaka 14 ya ujenzi, mradi ambao umekuwa ukizua mvutano mkubwa na mataifa ya chini ya mto—Misri na Sudan—kuhusu namna ya kujaza na kuendesha bwawa hilo.