Soko la mafuta duniani limeingia katika kipindi kipya cha taharuki baada ya kuongezeka kwa migogoro ya kijeshi katika maeneo mawili muhimu yanayohusiana na biashara ya nishati, huku mapigano kati ya Marekani na Iran pamoja na mashambulizi ya Ukraine dhidi ya meli za mafuta za Rusia yakiongeza hofu ya usumbufu wa usambazaji.

Katika athari zake, bei ya mafuta ghafi, ambayo ni kipimo muhimu cha soko la dunia, imepanda kutoka takribani dola 74.16 kwa pipa (sawa na takribani Sh200,000) hadi kufikia dola 84.95 kwa pipa (takribani Sh 229,000), kiwango cha juu zaidi ndani ya karibu mwezi mmoja.

Mlango huo hupitisha karibu asilimia 20 ya mafuta yote yanayosafirishwa duniani kwa njia ya bahari, hivyo tishio lolote la kijeshi katika eneo hilo huathiri moja kwa moja matarajio ya wafanyabiashara na wawekezaji wa nishati wakiwemo wa Tanzania.

Athari za mapigano hayo tayari yamekwisha tokea nchini Tanzania kwa gharama za bei mbalimbali kupanda ikiwemo mafuta yenyewe na bidhaa zinazotegemea nishati hiyo kusafirishwa kama vyakula.

Wakati hali hiyo ikiendelea, Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema operesheni za kijeshi dhidi ya Iran zitaendelea hadi pale vitisho dhidi ya masilahi ya Marekani na usalama wa njia za baharini vitakapokoma.

“Hatutakubali Iran kuhatarisha uhuru wa usafiri katika Hormuz au usalama wa washirika wetu,” Trump alinukuliwa akisema wakati akitangaza hatua mpya za kijeshi na kiusalama katika eneo la Ghuba.

Kwa upande wake, Iran imesisitiza haitasalimu amri mbele ya mashinikizo ya kijeshi, huku viongozi wake wakionya mashambulizi zaidi yanaweza kuathiri usalama wa usafirishaji wa baharini na miundombinu ya nishati katika eneo la Ghuba.

Hofu ya soko imeongezwa pia na vita vya Rusia na Ukraine baada ya Jeshi la Ukraine kutangaza kuzishambulia meli mbili za mafuta za Rusia katika Bahari Nyeusi, likisema meli hizo zilikuwa zikisaidia shughuli za kijeshi za Moscow.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ukraine, mashambulizi hayo yalilenga pia kreni ya mizigo katika Bahari ya Azov, huku Kyiv ikisema shabaha hizo zilihusishwa na operesheni za kijeshi za Russia.

Hatua hiyo imeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa njia za usafirishaji wa nishati katika eneo la Bahari Nyeusi, ambalo pia ni sehemu muhimu katika biashara ya mafuta na bidhaa nyingine duniani.

Wachambuzi wa masoko ya nishati wanasema bei kupanda hakusababishwi pekee na upungufu wa mafuta uliokwishatokea, bali zaidi na hofu ya kile kinachoweza kutokea endapo migogoro itaendelea na njia muhimu za usafirishaji zitaathirika.

Benki ya uwekezaji ya Goldman Sachs, taasisi kubwa ya kimataifa ya huduma za kifedha yenye makao yake Marekani, imeonya kuwa endapo usafirishaji kupitia Mlango wa Hormuz utavurugika kwa kiwango kikubwa, bei ya Brent inaweza kupanda hadi zaidi ya dola 110 kwa pipa (takribani Sh297,000).

Kwa Tanzania na nchi zinazoendelea, athari za mabadiliko hayo zinaweza kujitokeza kupitia gharama za kuagiza mafuta.

Hii ni kutokana na utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje, hali ambayo hufanya bei za ndani kuathiriwa na mwenendo wa soko la dunia.

Kupanda huko kwa bei ya mafuta kunaweza kuongeza gharama za usafirishaji wa bidhaa, uzalishaji viwandani na huduma nyingine zinazotegemea nishati ya mafuta, hali inayoweza kuathiri pia gharama za maisha ya wananchi.

Wataalamu wa uchumi wamekuwa wakishauri kuwa migogoro ya kijeshi katika maeneo muhimu ya uzalishaji na usafirishaji wa mafuta inaonyesha umuhimu wa nchi kuimarisha akiba ya kimkakati ya mafuta, kupanua matumizi ya gesi asilia na nishati mbadala.

Kwa sasa, macho ya dunia yameelekezwa kwenye maeneo yenye migogoro. Endapo mapigano yataendelea na njia za usafirishaji wa mafuta zitaendelea kuwa hatarini, bei zinaweza kuendelea kupanda.

Lakini juhudi za kidiplomasia zikifanikiwa kupunguza mvutano, masoko yanaweza kurejea katika utulivu na kushusha mshituko wa gharama hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *