Dar es Salaam. Wakati matumizi ya Akili unde (AI) yakizidi kubadili namna biashara zinavyoendeshwa duniani, sekta ya hoteli na ukarimu barani Afrika imeanza kuingia katika wimbi hilo huku wataalamu wakisema teknolojia hiyo inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kuongeza mapato, kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza ushindani wa biashara.

Mwelekeo huo umeonekana nchini Rwanda ambako viongozi wa hoteli, wamiliki wa biashara za ukarimu, mameneja wakuu na wakuu wa idara walikutana katika AI Masterclass iliyoandaliwa na Koncept AI Academy, wakijifunza namna ya kutumia AI katika shughuli za kila siku za uendeshaji wa hoteli.

Katika mafunzo hayo yaliyofanyika mwishini mwa wiki, washiriki walielekezwa jinsi teknolojia ya AI inavyoweza kusaidia kuboresha uzoefu wa wateja, kuongeza ufanisi wa wafanyakazi, kuimarisha kampeni za masoko, kuchambua taarifa za biashara kwa haraka na kusaidia viongozi kufanya uamuzi unaotegemea takwimu badala ya makisio.

Wataalamu wa teknolojia wanaeleza ukarimu ni miongoni mwa sekta zinazoweza kunufaika zaidi na AI kutokana na utegemezi wake mkubwa wa huduma kwa wateja, usimamizi wa taarifa na ushindani wa soko.

Kupitia AI, hoteli zinaweza kutabiri uhitaji wa wateja kulingana na misimu, kupanga bei kulingana na mabadiliko ya soko, kujibu maswali ya wateja saa 24 kupitia wasaidizi wa kidijitali (chatbots), pamoja na kuboresha usimamizi wa rasilimali na gharama za uendeshaji.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo mwishoni mwa wiki, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, Dk Krantz Mwantepele, alisema lengo la taasisi hiyo si kufundisha matumizi ya teknolojia pekee, bali kuwajengea viongozi uwezo wa kuitumia AI kama nyenzo ya kuongeza tija na ushindani wa biashara.

“AI si teknolojia ya kesho tena, ni nyenzo ya biashara ya leo. Tunataka viongozi waone namna inavyoweza kuongeza ufanisi, kuboresha huduma kwa wateja na kufungua fursa mpya za ukuaji wa biashara,” alisema.

Bara la Afrika lina nafasi kubwa ya kunufaika na mapinduzi ya AI ikiwa taasisi na kampuni zitawekeza katika kujenga uwezo wa viongozi na wafanyakazi wake.

“Kupitia Koncept AI Academy tunapeleka elimu ya vitendo na mageuzi ya AI kote Afrika na nje ya bara. Tunataka kuwawezesha viongozi, biashara, taasisi na serikali kuwa na maarifa na uwezo wanaohitaji ili kushindana katika dunia inayoendeshwa na AI,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwantepele, mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuharakisha matumizi ya AI katika sekta mbalimbali za uchumi ili taasisi zisibaki kuwa watazamaji wa mapinduzi ya teknolojia yanayoendelea duniani.

Mbali na kutoa mafunzo, ziara ya Koncept AI Academy nchini Rwanda imefungua milango ya ushirikiano na taasisi mbalimbali za elimu, sekta binafsi na wadau wa maendeleo. Miongoni mwa taasisi zilizoshiriki mazungumzo hayo ni Mount Kigali University, Royal FM, Paramount Kigali Hotel pamoja na wadau kutoka serikalini.

Ushirikiano huo unatarajiwa kusaidia kuendeleza programu za elimu ya AI, kujenga uwezo wa taasisi na kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za uchumi.

Wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa matumizi ya AI katika sekta ya huduma yanaweza kusaidia biashara kuongeza tija bila kuongeza gharama kubwa za uendeshaji, jambo linaloweza kuongeza ushindani wa kampuni za Afrika katika soko la kimataifa.

Kwa upande wa sekta ya hoteli, AI inaweza kutumika kuchanganua tabia za wateja, kuboresha huduma zinazotolewa kulingana na mahitaji yao, kupanga ratiba za wafanyakazi kwa ufanisi zaidi, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma.

Koncept AI Academy ilieleza kuwa itaendelea kuendesha masterclass za kisekta, programu za viongozi na mafunzo ya kujenga uwezo katika nchi mbalimbali za Afrika, ikiwa na lengo la kuziba pengo kati ya kasi ya maendeleo ya AI duniani na matumizi yake halisi katika biashara, taasisi na serikali.

Mwantepele alisema mafanikio ya programu hiyo nchini Rwanda yanaonesha kuwa uhitaji maarifa ya AI yanaongezeka kwa kasi, huku viongozi wengi wakitafuta njia za kuingiza teknolojia hiyo katika shughuli zao za kila siku.

“Afrika haipaswi kuwa mtumiaji wa AI pekee. Afrika lazima iongoze. Bara letu lina vipaji, ubunifu na fursa ya kuwa sehemu muhimu katika kuunda mustakabali wa AI duniani. Dhamira yetu ni kusaidia kugeuza uwezo huo kuwa matokeo halisi,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *