
Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imeonya utawala wa Saudi Arabia kuhusu “matokeo mabaya na makubwa” iwapo utaendelea kuongeza mashambulizi yake kwa kulenga miundombinu ya kiraia, na kuimarisha sera ya kuzingira bandari na viwanja vya ndege nchini Yemen.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu usiku, wizara hiyo imesisitiza kuwa: “Utawala wa kijinai wa Saudia lazima ukomeshe uchokozi na mzingira dhidi ya nchi yetu, vinginevyo utakabiliwa na matokeo yake.”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unaichukulia Jamhuri ya Yemen kama eneo lililo chini ya udhibiti na ulinzi wake. Wizara hiyo ilisema, “Kama utawala huo ungekuwa na nia ya dhati kuhusu mamlaka na uhuru wa Yemen, ungetangaza kuondoka kwake kikamilifu nchini. Hii inatokea huku utawala wa kijinai wa Saudia ukituonyesha majivuno na dharau kila wakati unaporuhusu meli zake za chakula na dawa kutia nanga katika bandari za Yemen.”
Wizara hiyo imesisitiza kuwa Wayemen hawajasahau na hawatasahau mauaji ya halaiki ya makumi ya maelfu ya raia, hususan wanawake na watoto, yaliyotokana na uchokozi wa Saudia katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.
Aidha wizara hiyo imesisitiza kuwa mamlaka ya Saudia inapaswa kutambua kuwa hali iliyopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mfalme Khalid mjini Riyadh inapaswa kuwa sawa na ile ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sana’a, na kwamba hali ya miji ya bandari ya Yanbu na Jizan kwenye pwani ya Bahari ya Sham inapaswa kuwa sawa na ile ya Bandari ya Hudaydah nchini Yemen.
Taarifa hiyo iliongeza: “Utawala wa kijinai na usio na busara wa Saudia lazima ufahamu kuwa kurejea kwenye njia ya haki, uadilifu, na usawa ni nafuu zaidi kuliko kushikilia njia potovu ya uchokozi.”
Siku ya Jumatatu, Yemen ilitangaza “mzingiro wa baharaini” dhidi ya Saudi Arabia kuanzia sasa.
Msemaji wa Jeshi, Brigedia Jenerali Yahya Saree, alisema katika taarifa iliyorushwa kwenye televisheni kwamba marufuku ya kupita meli zinazohusiana na Saudia “imeanza kutekelezwa kuanzia wakati huu taarifa hii ilipotolewa.”
Brigedia Jenerali Saree alionya kuwa hatua yoyote ya kuongeza uhasama na Saudia itajibiwa kwa “vikali na kwa upana.”