MSHAMBULIAJI Jonathan Sowah amewasili nchini tayari kwa kurejea klabu yake ya zamani ya Singida Black Stars lakini wakati akitangaza hesabu zake mpya kwenye soka la Tanzania akaizungumzia Simba kwa maneno ambayo mashabiki wa wekundu hao yatawafikirisha.
Sowah baada ya kuachana na Simba iliyompa ‘Thank You’ na yeye kuwaaga amerejea nchini akienda kujiunga na Singida ambayo ndio iliyomleta nchini kisha baadaye kuwagawia wekundu hao msimu uliopita.
Akizungumza baada ya kuwasili Sowah amesema, anarejea Tanzania kurudisha ubora wake ambao alionyesha wakati anajiunga na Chui hao wa Singida, akisema anataka kufanya makubwa na klabu hiyo kuanzia msimu ujao.
Sowah amesema hana shida na Simba na ameshazitupa kurasa mbaya alizopitia wakati akiwa na wekundu hao na kwamba sasa anarejea Tanzania akifuata ligi yenye ushindani na kuitumikia klabu ambayo anaiheshimu kwa viongozi wake kujali maisha yake.
Kabla ya kutua Simba Sowah alicheza nusu msimu tu akifunga mabao 13 akionyesha kiwango kikubwa cha kufunga mabao kisha msimu uliopita mwanzoni wekundu hao wakamsajili lakini, akufanya makubwa akiishia kufunga mara tatu pekee.
Hata hivyo, mshambuliajio huyo baadaye akaingia kwenye mgogoro na wekundu hao mpaka kufikia hatua ya kusimamishwa ambapo kuanzia hapo hakurejea tena kuwatumikia Simba na kurejea kwao Ghana.
“Nimerudi hapa, nimerudi kuja kujiunga tena na familia yangu ya Singida, unafahamu hii ndio timu iliyonileta hapa kwa gharama kubwa sana kabla, nilichotakiwa kufanya ni kuwatumia kwa nguvu na nikafanya hivyo ule msimu wangu wa kwanza hapa,”amesema Sowah.
“Sitaki kufikiria yaliyotokea hapa kati wakati nikiwa Simba, sina shida nao, nimeziweka kando kurasa mbaya nilizopitia lakini sasa nataka kuwa na mwanzo mwingine, najipanga kuhakikisha viongozi wa Singida ambao wanaamini uwezo wangu wananufaika na maamuzi yao.
“Nataka kazi yangu izungumze uwanjani kuliko mdomo wangu kama ambavyo nilifanya wakati nafika hapa mara ya kwanza, nadhani mtamuona Sowah mshindani uwanjani ambaye narudi kuipigania heshima ya klabu na yangu binafsi.
“Ligi ya hapa ni ligi yenye ushindani sana ndio maana unaona wachezaji wakubwa wanakuja hapa, ukipata nafasi ya kucheza hapa unaridhika kwamba timu zinashindana kweli, naweza kusema ndio kitu ambacho kimechangia kurejea kwangu hapa.”
Sowah baada ya kufika nchini alisafirishwa haraka kuiwahi timu yake ya Singida ambayo atakutana nayo njiani ikielekea nchini Rwanda, kwenye mashindano ya Kombe la Kagame ambalo Chui hao ndio mabingwa watetezi.