Morogoro. Serikali imesema itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini sambamba na kufanya maboresho ya kanuni za kodi ili kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 21,2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, wakati akifungua kongamano la kitaifa la ubunifu na kongani, lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na kongani, vituo atamizi, watafiti na wanazuoni, wajasiriamali, sekta binafsi pamoja na taasisi za kifedha.

Londo amesema Serikali imeendelea kutekeleza mageuzi mbalimbali yenye lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, ikiwemo kufanya marekebisho ya kanuni 374 za kodi kufuatia mapendekezo ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Mfumo wa Kodi.

Amesema miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha wawekezaji wanaowekeza katika maeneo yenye changamoto au yasiyo na faida kubwa wanapatiwa mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji, ikiwemo kuimarisha usalama na kuweka sera zinazowezesha shughuli zao kufanyika kwa ufanisi.

Londo amesema hatua hizo zinalenga kuongeza ushindani wa uchumi, kuchochea ubunifu, kuvutia uwekezaji zaidi na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya Taifa.

 “Bunifu hizi pamoja na uwekezaji kwenye kongani mbalimbali zitatoa ajira kwa vijana na kufungua fursa nyingine za kiuchumi, hivyo kama Serikali tutaendelea kushirikiana na wadau wengine kama Sido (Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo), TBS (Shirika la Viwango Tanzania), Tirdo (Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania) na taasisi za fedha kuhakikisha tafiti zinafanyika na hizi bunifu zinaendelezwa,” amesema Londo.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa Serikali itaendelea kulinda ujuzi na bunifu mbalimbali za vijana ili zisiweze kutoweka kwa kuwa zinachangia kukuza uchumi wa nchi na kuchangia kwenye sekta ya ajira.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadar Singo amesema kuwa jukumu la taasisi hiyo ni kutoa mafunzo kwa viongozi, kufanya tafiti tumizi, kuandaa mijadala ya kisera, pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi za umma na binafsi.

Wadau walioshiriki kwenye kongamamo la kitaifa la ubunifu na kongani mkoani Morogoro lililoandaliwa na taasisi ya Uongozi na kuzishirikisha kongani, vituo atamizi, watafiti na wanazuoni, wajasiliamali, sekta binafsi na taasisisi za kifedha. Picha Hamida Shariff

Ameongeza kuwa wanafanya hivyo kwa kuamini kwamba uongozi bora haujengwi kwa mafunzo pekee, bali pia kwa kuzalisha maarifa, kuyajadili na kuyatafsiri kuwa sera na hatua zinazoweza kuleta matokeo chanya kwa Taifa.

Singo amesema kuwa kongamano hilo ni matokeo ya mchakato wa kitaaluma ulioanza mwaka wa fedha uliopita ambapo Taasisi ya Uongozi, kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, ilifanya utafiti kuhusu mchango wa vituo vya ubunifu na kongani za biashara katika kukuza biashara ndogo na za kati nchini Tanzania.

Amesema utafiti huo umelenga kuelewa mchango wa vituo vya ubunifu na kongani za biashara katika kukuza ujasiriamali, kuongeza ubunifu, kurahisisha upatikanaji wa teknolojia, mitaji, masoko na huduma za ushauri kwa biashara ndogo na za kati.

“Hata hivyo, utafiti wetu pia umeonesha kuwa bado kuna changamoto nyingi zinazopunguza uwezo wa vituo hivi kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Singo.

Amefafanua kwamba changamoto hizo haziwezi kutatuliwa na taasisi moja peke yake, ndiyo maana wamekutana kwa ajili ya kujadili kwa pamoja na kuzipatia majawabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza amesema kuwa asilimia 78 ya biashara hapa nchini zinaendeshwa nje ya mfumo rasmi hivyo ameiomba Serikali kupitia hiyo kuweka mifumo inayosomana kuondoa usumbufu wa kibiashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *