Inakadiriwa kuwa watu milioni 645 walikumbwa na njaa mwaka jana duniani kote; idadi ambayo ni pungufu kwa watu milioni 14 ikilinganishwa na mwaka 2024, na wakati huo huo ni pungufu kwa watu milioni 43 ikilinganishwa na idadi ya watu walioathiriwa na njaa mwaka wa 2022. Takwimu hizi ni kwa mujibu wa ripoti ya karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani.

Hata hivyo, mamia ya mamilioni ya watu wanaendelea kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula unaosababishwa na migogoro, misukosuko ya kiuchumi na hali mbaya ya hewa iliyokithiri.

Kulingana na ripoti iliyochapishwa siku ya Jumanne, inakadiriwa kuwa asilimia 7.8 ya watu duniani walikabiliwa na njaa mwaka wa 2025, kiwango ambacho ni cha chini ikilinganishwa na asilimia 8.1 mwaka wa 2024, na asilimia 8.6 mwaka wa 2022.

Kupungua huku kunaashiria mwaka wa tatu mfululizo wa nafuu baada ya njaa kuongezeka sana wakati wa janga la COVID-19. Hata hivyo, viwango vya njaa bado ni vya juu kuliko vilivyokuwa mwaka wa 2019, kabla ya janga hilo kutokea.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imeitaja Afrika kuwa eneo linaloendelea kuwa na kiwango cha juu zaidi cha njaa duniani.

Mwaka 2025, ilikadiriwa kuwa watu milioni 309 barani Afrika waliathiriwa na utapiamlo; idadi ambayo ni sawa na mtu mmoja kati ya watu watano barani humo, na inayowakilisha karibu nusu ya watu wenye njaa duniani.

Kwa kulinganisha, ripoti ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, watu milioni 292 barani Asia (ambayo ni sawa na asilimia 6 ya idadi ya watu); na milioni 32 huko Amerika ya Kusini na Karibea walikumbwa na utapiamlo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *