
Maandamano yaliyoitishwa na muungano wa upinzani wa C64 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kupinga mpango wa kuibadilisha katiba hayatafanyika tena leo Jumatano baada ya kuahirishwa kufuatia wito wa kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hatua hii imezua mitazamo mbalimbali miongoni mwa wapinzani.
Viongozi wa dini, wakiongozwa na Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki CENCO na madhehebu ya Kiprotestanti, yamepewa kazi ya kuongoza mazungumzo hayo, na ndio waliomba upinzani kuahirisha maaandamano ya Julai tarehe 22.
Kulikuwa na mikutano kadhaa, iliyosababisha muungano wa C64 kukukubali kuahirisha maandamano yao, licha ya kuwepo kwa upinzani mkali miongoni mwao.
Miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliopinga kuahirishwa kwa maandamano hayo ni Seth Kikuni, kutoka muungano wa kuukoa DRC, unaomuunga mkono rais wa zamani Joseph Kabila. Kikuni anasema, lilikuwa kosa kubwa kwa viongozi wa C64 kukubali kuahirisha maandamano hayo.
Dominique Munongo, kutoka chama cha Ensemble chake Moise Katumbi naye amepinga kuahirishwa kwa maandamano hayo anayosema yalipaswa kuendelea ili kumpa shinikizo rais Tshisekedi.
Hata hivyo, Ferdinand Kambere Naibu Katibu mkuu wa chama cha PPRD chake rais wa zamani Joseph Kabila yeye amesema mazungumzo yapewe nafasi, lakini wapinzani wawe macho.