Tulianza kuwaona mabaunsa enzi za majumba ya sinema na disko. Baadaye kidogo tuliona kwenye muvi za wazungu, mabaunsa wakichukua nafasi za walinzi binafsi au mabodigadi.

Naikumbuka ile ambayo wafanyabiashara wanaelewana halafu wanalindwa na mabodigadi waliokuwa mahasimu wakubwa, kama sikosei walikuwa Arnold Schwarzenegger na Bollo Yeung. Kila baada ya kazi walitafutana kwa kiu kubwa ya mapigano.

Kwa mtindo huo, mabodigadi walionesha kushughulika na maslahi binafsi badala ya kile kilichowaweka kazini. Na huu ndio ukweli wa mambo yanavyotokea, baada ya shughuli za kulinda amani kutekelezwa na watu wasio na mafunzo maalum.

Wakati mwingine watu wa aina hii hujijngiza kwenye mifumo rasmi, lakini wanafanya mambo kinyume cha sheria bila kuzingatia utu wa wanayemshughulikia.

Kumekuwa na taarifa za migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali, ambapo wananchi wanadai walinzi binafsi waliokuwa wakilinda shughuli za wawekezaji au watekelezaji wa amri za kubomoa, walihusika na matumizi ya nguvu kupita kiasi, pamoja na madai ya kuporwa mali wakati wa ubomoaji.

Baadhi ya matukio hayo yaliibua malalamiko kutoka kwa wananchi na mashirika ya kutetea haki za binadamu.

Kinyume na askari wenye mafunzo, mabaunsa hutumia vipigo na kutumia nguvu kupita kiasi: Baadhi ya waathirika wamekuwa wakipigwa na kuburutwa bila sababu za msingi.

Ni vigumu sana mtu anayeshughulikiwa kutambua iwapo amewekwa chini ya ulinzi au yupo hatarini, kwa sababu hawa jamaa zetu hawajui au hawatumii mbinu za mafunzo ya kitaalamu. Mbinu zao zinaweza kupelekea mauaji au majeraha bila ulazima wowote.

Kama vile haitoshi, mabausa huingia kwenye makabati na sehemu zingine kupora mali za muathirika.

Kitu hicho ndicho kinachotuhakikishia kuwa hawa si walinzi wa amani, bali ni watu waliojificha kwenye kivuli cha kazi kwa malengo ya unyanyasaji na wizi. Matukio yao yamejawa na uharibifu wa mali na upotevu wa fedha. Kwenye tukio moja inasemekana waliiba mpaka marashi ya mwenye nyumba!

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa za kijana aliyekamatwa na kuhojiwa na mabaunsa. Jambo la kwanza hawakujitambulisha kwake, ila walianza kumsakama kwa tuhuma ambazo mwenyewe hakuzijua.

Mahojiano hayo yasiyo rasmi yalitawaliwa kwa kiasi kikubwa na vipigo visivyokuwa na kiasi. Walimfanyia hivyo kwa muda mrefu hatimaye mtoto wa watu akapoteza maisha mikononi mwao.

Katika siku za nyuma kulikuwa na wimbi la makomandoo wa vyama vya siasa. Walitokana na Jumuiya za vijana wa vyama hivyo, wakajipa kazi ya kulinda viongozi wao kwa mitindo waliyoibuni wenyewe.

Matokeo yake hayakuwa mazuri kwani walimshughulikia kila waliyemhisi kuwahujumu kwa namna waliyojipangia.

Serikali iliwapiga marufuku na kuwaagiza waliachie Jeshi la Polisi lifanye kazi yake.

Baadaye waliibuka “watu wasiojulikana” waliokuwa wakikamata bila utaratibu. matukio yalianza kwa watu walikamatwa na kupelekwa kusikojulikana, yakaunganika na upotevu wa raia na watoto wasio na hatia.

Nchi iliingia kwenye taharuki maana kila mmoja hakuwa na uhakika na usalama wake. Mbaya zaidi, hakuna aliyekamatwa na kujulikana kwa mzizi wa magenge yao. Hadi hivi sasa kuna watu waliopotea bila kuonekana.

Kwa jinsi inavyoonekana, makundi ya mabausa, makomandoo na watekaji yana mahusiano. Ni sawa na mwizi unayemfungia geti akatafuta upenyo kwenye uzio. Binadamu wote wanatafuta ili kujikimu na familia zao, japo wezi wanatafuta kwa njia haramu.

Jeshi la Polisi linaingiliwa na watu wasiojulikana. Ni jukumu kobwa kwa Jeshi hilo kufanya uchunguzi wa chanzo cha haya yote. Njia sahihi ni kuwakamata na kuwahoji kwa kina ili kuvumbua chimbuko lao na nani anayewatuma. Kama hilo linahuwa gumu kwao, wanao uwezo wa kuomba msaada wa ndugu zao waliofanikiwa kuyadhibiti mambo kama hayo.

Nina uhakika na ushirikiano wa majeshi katika kanda zetu hadi kimataifa.

Sisi hatuamini sana neno la “watu wasiojulikana”. Enzi zetu huku uswahilini kulikuwa na wahuni. Ilikuwa ni lazima mwizi wa Ilala anapokuja Chang’ombe Unubini, aripoti kwa kiongozi wa wezi wa pale. Pengine sio mfano mzuri huu ninaoutoa, lakini kulikuwa na nidhamu hiyo hata kwa wahalifu. Mtu yeyoye huwa hajulikani kwa wasiomjua.

Mkitaka kumjua anzeni na wanaomjua.

Kwa muktadha huu, ni dhahiri kuwa changamoto ya mabaunsa na makundi yasiyo rasmi ni tishio kwa ustawi wa jamii. Haiwezekani mtu akaamua tu awe anavyotaka bila kufuata utaratibu.

Wavunjaji wa sheria wanapojipa mamlaka bila mafunzo, huifanya kazi yao vibaya na matokeo huwa ni madhara makubwa kwa raia wasio na hatia. Haki za binadamu hukiukwa, mali hupotea, na maisha huangamia.

Ili kurejesha imani ya wananchi, ni lazima Jeshi la Polisi na vyombo vya dola viimarishe uwajibikaji, vionyeshe uwazi na kushirikiana na jamii.

Aidha, elimu ya uraia na nidhamu ya kijamii ni nguzo muhimu za kuzuia uhalifu wa kivuli. Tukikumbatia mshikamano na kuimarisha taasisi rasmi, tunaweza kuondoa hofu ya mabaunsa na kujenga taifa lenye amani, usalama na heshima kwa utu wa kila mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *