
Rais wa Marekani, Donald Trump, anataka kumteua Rais wa FIFA, Gianni Infantino katika nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Tovuti ya gazeti la New York Post, ikinukuu chanzo kilicho karibu na Rais wa Marekani Donald Trump, imefichua kwamba kiongozi huyo anataka Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Gianni Infantino awe Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Trump anaamini kwamba Infantino “anaheshimiwa sana kimataifa na ana uwezo wa kuwaunganisha watu, jambo ambalo linamfanya astahili nafasi hiyo.”
Bado haijabainika iwapo Infantino anataka kugombea nafasi hiyo au la.
Tovuti hiyo imeeleza kuwa jina la Infantino linapigiwa debe kutokana na uhusiano wake wa karibu na Trump wakati wa kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia FIFA 2026 nchini Marekani, ambapo wawili hao walionekana pamoja mara kadhaa, na kila mmoja akisifu mchango wa mwenzake katika kufanikisha mashindano hayo.
Muhula wa pili wa Katibu Mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, umepangwa kumalizika Desemba 31, huku nchi wanachama zikianza taratibu za kumchagua mrithi wake kwa mujibu wa taratibu zinazotumika ndani ya shirika hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa huchaguliwa kwa pendekezo la Baraza la Usalama, kabla ya uteuzi huo kuidhinishwa na Baraza Kuu.
Ni vyema kukumbusha kuwa, Rais wa FIFA, Gianni Infantino anakabiliwa na uwezekano wa uchunguzi wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa kufuatia malalamiko yanayomtuhumu kwamba amekiuka kanuni ya kutopelea upande wowote kisiasa kwa kumuunga mkono Donald Trump.
Shirika la kutetea haki za binadamu FairSquare limetangaza kuwa litawasilisha malalamiko kwa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa kuhusu kile lilichosema ni “ukiukwaji wa mara kwa mara wa sheria za kutopendelea upande wowote kisiasa” wa Infantino.
FairSquare ilikuwa imewasilisha malalamiko ya awali kwa Kamati ya Maadili ya FIFA mnamo Desemba 2025, ikitaja matukio mengi mfululizo ambapo Infantino alielezea “uungaji mkono wa waziwazi kwa vitendo na sera” za Donald Trump.
Aidha, FairSquare imetaja uamuzi wa Infantino wa kumtunza Trump tuzo ya kwanza ya amani ya FIFA (FIFA Peace Prize) kama sehemu ya malalamiko yake. Shirika hilo limeitaka FIFA kuchunguza iwapo uundaji wa tuzo hiyo na kukabidhiwa kwake kwa kiongozi wa kisiasa aliyeko madarakani unaendana na sheria za kutofungamana na siasa za shirikisho hilo.
Wakosaji wa tuzo hiyo wameelekeza kidole kwenye rekodi ndefu ya Donald Trump ya ukiukaji wa haki za binadamu na maamuzi yenye utata, ikiwa ni pamoja na mizozo ya sera zake za kigeni, hatua kali dhidi ya wahamiaji, uvamizi wa Marekani dhidi ya Venezuela, ushiriki wa serikali ya Trump katika mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza, mashambulizi ya kinyama dhidi ya Iran na kesi za kisheria zinazomkabili, kama sababu zilizofanya tuzo hiyo kukosolewa vikali.