Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, ameikosoa serikali ya Kuwait kwa kile alichokiita kutokuwa na shukrani nchi hiyo na kuwakaribisha maadui wa Iran licha ya uhusiano wa ujirani uliopo kati ya nchi hizo.

Baqaei amesema hatua ya Kuwait ya kuwapa nafasi watu au makundi yanayochukua misimamo ya uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiendani na misingi ya uhusiano mwema wa ujirani na ushirikiano wa kikanda.

Aidha, amesisitiza kuwa Iran inatarajia nchi jirani kuzingatia kanuni za kuheshimiana, kutohujumiana na kutoruhusu maeneo yao kutumiwa kwa shughuli zinazohatarisha usalama na maslahi ya nchi nyingine katika eneo hili.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amekumbushia msaada wa kihistoria wa Iran ilioitoa kwa Kuwait wakati wa uvamizi wa utawala wa Saddam Hussein dhidi ya nchi hiyo.

Baqaei amekosoa hatua ya Kuwait ya kuwakaribisha maadui wa Iran na kushirikiana nao katika kuchochea uadui dhidi ya wananchi wa Iran, akisema kuwa kitendo hicho kinaonyesha kutokuwa na shukrani nchi hiyo kwa msaada wa kihistoria ambao Iran iliitoa, pamoja na kukosa mtazamo wa mbali kuhusu mustakabali wa uhusiano kati ya nchi hizo.

Esmaeil Baqaei amechapisha ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X, akiwa ameambatanisha picha ya wataalamu wa Iran waliokwenda Kuwait mwaka 1991 kuzima moto wa visima vya mafuta vilivyokuwa vikiteketea.

Baqaei ameandika kuwa, picha hiyo ya kihistoria inaonyesha wataalamu wa Iran wenye kujitolea waliokwenda kusaidia kuzima moto wa visima vya mafuta vya Kuwait baada ya jeshi la utawala wa Baath wa Iraq kujiondoa nchini humo mwaka 1991.

Alisema hatua hiyo inaonyesha nafasi ya Iran katika kusaidia nchi jirani wakati wa matatizo, akisisitiza kuwa kumbukumbu za matukio kama hayo zinapaswa kuzingatiwa katika uhusiano wa sasa kati ya mataifa ya eneo hili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *