Zaidi ya vipande 62 vya miili ya wanafunzi 32 waliouawa katika shambulio la anga la Marekani katika Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyebeh huko Minab kusini mwa Iran vimetambuliwa kupitia vipimo vya vinasaba (DNA) na kuzikwa, karibu miezi mitano baada ya mashambulizi yaliyoua wanafunzi na walimu wao wasiopungua 168.
Mabaki hayo, yaliyopatikana kufuatia wiki kadhaa za shughuli za utafutaji katika Shule ya Shajareh Tayyebeh na maeneo ya jirani, yamesindikizwa leo Jumatano katika mkoa wa Hormozgan katika msafara wa mazishi kabla ya kuzikwa katika makaburi ya mashahidi wa mji huo.
Wazazi waliokuwa na huzuni na raia wengine walikusanyika mapema katika eneo ambako majeneza yaliandaliwa ili kuaga mabakii ya watoto hao.
Mojtaba Qahramani, mkuu wa Idara ya Mahakama ya Hormozgan, amesema kwamba licha ya shughuli nyingi maalumu za utafutaji katika shule hiyo na viunga vyake, hakuna dalili yoyote iliyopatikana ya Makan Nasiri mwenye umri wa miaka 7, mwanafunzi wa darasa la kwanza, mhanga pekee ambaye mwili wake haujapatikana hadi sasa.
Qahramani ameliambia shirika la habari la Fars kwamba kombora la Marekani lilipiga moja kwa moja mahali ambapo Makan alikuwa amesimama wakati wa mashambulizi dhidi ya shule ya Minab.

Kaburi tupu limeandaliwa kwa ajili ya Makan, huku vifaa vyake binafsi, ikiwemo sweta yenye madoa ya damu na kiatu kimoja cha raba alizokuwa amevaa, vikihifadhiwa kwenye sanduku la kioo kwenye msikiti ulio karibu na shule hiyo.
Wazazi wake wametumia miezi kadhaa wakitafuta alama yoyote ya mwana wao bila mafanikio. “Nitamtafuta wapi mwanangu?” baba yake aliuliza katika mahojiano na vyombo vya habari mapema mwaka huu, macho yake yakitiririka machozi.
Shambulio la Februari 28 katika Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyebeh lilitokea siku ya kwanza ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran na linatambuliwa kuwa shambulio baya zaidi la vita vya kigaidi dhidi ya raia.
Uchunguzi unaonyesha kuwa makombora matatu ya Tomahawk ya Marekani yalitumiwa kushambulia moja kwa moja shule hiyo. Shule hiyo ilipigwa mara tatu tofauti.
Mashambulizi hayo yamelaaniwa na Umoja wa Mataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu. “Familia za wasichana wadogo waliouawa zina haki ya kujua ukweli wa jinsi jambo hilo lilivyotokea,” alisema Ravina Shamdasani, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Vipande 62 vilivyozikwa leo Jumatano vilitambuliwa kuwa vya wanafunzi 32 wa Shule ya Msingi ya Shajareh Tayyebeh, kwa mujibu wa Gavana wa Minab, Mohammad Radmehr.