Naibu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Viwanda na Biashara, Aristides Mbwasi, amesema ujio soko jipya la YIWU Market ndani ya Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) Dar es Salaam, unalenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Tanzania na China.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa Soko hilo , amesema  uzinduzi huo unatekeleza dhamira ya viongozi wa mataifa hayo mawili ya kuendelea kukuza biashara, uwekezaji na diplomasia ya uchumi.

Mbwasi amesema Serikali imepongeza maendeleo makubwa ya EACLC tangu ilipozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka mmoja uliopita, akibainisha kuwa kituo hicho kimeendelea kuvutia wafanyabiashara kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.

Ameeleza kuwa zaidi ya maduka 190 tayari yamepata wapangaji, jambo linaloonyesha ongezeko kubwa la shughuli za biashara na imani ya wawekezaji katika kituo hicho.

Amesema soko hilo litasaidia wafanyabiashara wa Tanzania kupunguza gharama za safari za kwenda China kutafuta bidhaa, kwani sasa bidhaa hizo zitapatikana moja kwa moja nchini. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha bidhaa zote zinazouzwa katika soko hilo zinakidhi viwango vya ubora vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kulinda maslahi ya watumiaji.

Mbwasi pia amesema soko hilo limeandaa eneo maalumu la Made in Tanzania, litakalotumika kutangaza na kuuza bidhaa zinazozalishwa nchini katika soko la China na mataifa mengine. Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, ikiwemo mazao ya kilimo kama ufuta na soya ambayo tayari yanapata soko nchini China.

Ameongeza  kuwa YIWU Market siyo fursa kwa Tanzania pekee bali kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki, SADC na Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), ambapo Dar es Salaam inatarajiwa kuwa kitovu cha biashara za kikanda. Alibainisha kuwa kituo hicho kina huduma mbalimbali za taasisi za Serikali, ikiwemo TRA, zinazorahisisha uingizaji na usafirishaji wa bidhaa, hivyo kuongeza ufanisi wa biashara na uwekezaji.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kituo Cha Biashara na na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) Lissa Wang amesema ujio wa Soko la YIWI market utaidia wafanyabiashara wa Nchini na China kufanya Biashara kwa urahisi na tija zaidi .

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Katika Kituo Cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) Ayubu Katuga amesema ujio huo wa Soko itaendelea kurahisha ufanyaji wa Biashara zaidi hivyo kukuza Pato la taifa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *