Utawala wa Rais Donald Trump umeripotiwa kuanza kutafakari kutekeleza hujuma za kijeshi dhidi ya Mali, nchi ya Afrika Magharibi ambayo ni maarufu kwa utajiri mkubwa wa  dhahabu. Hatua hii, ikiidhinishwa, itaiongeza nchi hiyo katika orodha ndefu ya mataifa yaliyolengwa na Washington tangu Rais huyo mpenda vita kurejea madarakani mwaka jana.

Ripoti zinaonyesha kuwa maafisa wa Marekani wanashinikiza mashambulio hayo nchini Mali kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi lenye uhusiano na al-Qaeda, ambalo limedai kuhusika na mashambulio na utekaji nyara tangu kuundwa kwake mwaka 2017. Hata hivyo, wachambuzi wa mambo wanaona shaka katika simulizi hili, wakibainisha kuwa hatua hizi zinakuja wakati ule ule Washington ikiwa imezama katika vita vya miezi kadhaa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari vya Marekani, ikiwa mashambulio haya yataidhinishwa, yatapanua zaidi wigo wa uchokozi wa kijeshi wa Marekani chini ya muhula wa sasa wa Trump. Tangu mwaka 2025, vikosi vya Marekani vimekuwa vikitekeleza mashambulio katika nchi nyingi na maeneo ya bahari, hatua inayothibitisha sera ya uingiliaji kati inayopanuka, licha ya ahadi za mara kwa mara za Trump kumaliza vita vya nje.

Trump tayari ameidhinisha hatua za kijeshi nchini Iraq, Nigeria, Somalia, Syria, Venezuela, na Yemen. Operesheni hizo za Marekani pia zimehusisha kushambuliwa kwa vyombo vya usafiri vya baharini vinavyodaiwa kusafirisha dawa za kulevya katika maeneo ya Caribbean na Pasifiki ya Mashariki, operesheni zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 200.

Mali, ambayo inaongozwa na Jenerali Asimi Goita, ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa dhahabu barani Afrika, ni sehemu ya muungano wa kikanda wa serikali zinazoongozwa na kijeshi ambazo zinapinga ukolono mambo leo wa nchi za Magharibi. Nchi hizo ni Mali, Burkina Faso na Niger. Nchi hizo tatu zimepunguza kwa kiasi kikubwa mahusiano yao na madola ya Magharibi, hatua inayoonekana kukiuka maslahi ya Washington.

Hatua yoyote ya kijeshi ya Marekani nchini Mali itaongeza shinikizo kwa nchi hiyo yenye utajiri wa dhahabu na madini mengine yenye umuhimu kama vile uraniumu na lithium. Hali hii inazua maswali mapya kuhusu iwapo Marekani kweli inataka kuangamiza magaidi kama inavyodai, au kama ni sehemu ya maslahi mapana zaidi katika maeneo yenye umuhimu mkubwa wa kiuchumi na kimkakati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *