Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amelionya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC) pamoja na Jordan kwamba, ushiriki wowote katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran utachukuliwa kuwa ni kitendo cha uchokozi wa kijeshi.

Baqaei amesema kuwa, nchi yoyote itakayochangia au kuwezesha mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa namna yoyote ile, itakuwa imejihusisha moja kwa moja na kitendo cha uvamizi, jambo ambalo linapingana na sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Ameongeza kuwa Iran inasisitiza umuhimu wa kuheshimiwa mamlaka ya kitaifa na mipaka ya nchi, huku akizitaka nchi za eneo kujiepusha na hatua zozote zinazoweza kuongeza mvutano na kuhatarisha usalama na utulivu wa kanda.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amezitaka nchi tano wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC) pamoja na Jordan kukanusha rasmi madai ya Marekani kwamba zilishiriki katika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.

Baqaei ameyasema hayo baada ya kuchapisha video yenye kauli za Kamanda wa Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM), Jenerali Brad Cooper, ambaye anadai wazi kuwa nchi tano za Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na Jordan zilishiriki katika operesheni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran.

Ameongeza kuwa iwapo madai hayo ya Marekani si ya kweli, basi serikali za nchi zilizotajwa zinapaswa kuyakanusha hadharani kwa tamko rasmi na la wazi, ili kuondoa utata kuhusu nafasi na mchango wao katika hujuma ya kijeshi dhidi ya Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesema chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama na migogoro katika eneo la Asia Magharibi ni mashambulizi ya kijeshi yaliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baqaei amesisitiza kuwa, ushiriki wa aina yoyote katika mashambulizi hayo, ikiwemo kuruhusu ardhi, anga au miundombinu ya nchi kutumika katika operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, unahesabiwa kuwa kitendo cha uchokozi kwa mujibu wa azimio nambari 3314 la Umoja wa Mataifa linalofafanua maana ya uchokozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *