Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, ukimya na misimamo ya kindumakuwili kuhusu mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunawapa nguvu na kuwahamasisha wavamizi kuendelea kutekeleza vitendo vyao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), unaofanyika mjini Cholpon-Ata nchini Kyrgyzstan.

Katika hotuba hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na maendeleo ya kisiasa na kiusalama yanayoikabili dunia.

Araghchi amesema kuwa baada ya mashambulizi ya Juni 2025, dunia ilishuhudia tena kati ya Februari na Aprili 2026 mashambulizi mengine dhidi ya Iran, ambayo kwa mujibu wake hayakuhatarisha tu usalama wa taifa la Iran bali pia yalidhoofisha uhalali na hadhi ya mfumo mzima wa sheria za kimataifa.

Araghchi aliongeza kuwa tarehe 28 Februari 2026 ilikuwa miongoni mwa siku zenye majonzi makubwa katika historia ya Iran. Alisema siku hiyo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran, akiwa ni mamlaka ya juu zaidi ya kisiasa na kidini nchini humo, aliuawa pamoja na wanafamilia wake akiwa ndani ya ofisi yake, katika tukio alilolitaja kuwa ni shambulizi la kigaidi na ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema mashambulizi mengine yalilenga shule ya Shajareh Tayyibeh katika mji wa Minab na watu 168 waliuawa wakiwemo wanafunzi tukio ambalo ni uhalifu mkubwa dhidi ya raia.

Amesema matukio hayo hayakuishia hapo, akieleza kuwa siku hiyo hiyo uwanja wa michezo katika mji wa Lamerd, mkoani Fars, pia ulilengwa katika shambulio.

Kwa mujibu wa Araghchi, ushahidi wa kitaalamu na mabaki ya silaha zilizotumika unaonyesha kuwa shambulio hilo lilifanywa kwa kutumia silaha ambazo, zinapingana na misingi ya sheria za kimataifa za kibinadamu na zilitumika kwa mara ya kwanza dhidi ya raia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *