Dar es Salaam. Kajala Masanja na Harmonize wameibua mjadala mpya mitandaoni baada ya baadhi ya mashabiki kuanza kuhoji hatma ya uhusiano wao, huku wengine wakionyesha kuchoshwa na kile wanachokiita penzi la “kuachana na kurudiana.”
Baada ya kuonekana kurejesha ukaribu wao miezi kadhaa iliyopita na kuwapa matumaini mashabiki, sasa ukimya wao umeanza kuzua maswali mapya kuhusu hali ya uhusiano huo.
Kilichochochea zaidi mjadala huo ni kupita kwa siku ya kuzaliwa ya Kajala bila Harmonize kuweka ujumbe wa kumpongeza hadharani, tofauti na ilivyowahi kutokea nyakati zilizopita.
Ingawa hakuna kati yao aliyethibitisha kuvunjika kwa uhusiano huo, hali hiyo imewafanya baadhi ya mashabiki kuhisi huenda mambo si shwari nyuma ya pazia.
WALIREJESHA PENZI FEBRUARI
Kajala na Harmonize walionekana kurudisha ukaribu wao Februari mwaka huu baada ya kipindi cha ukimya kilichofuata taarifa za kutengana.
Hatua hiyo iliwafurahisha mashabiki waliokuwa bado wanaamini penzi lao linaweza kudumu, hasa kutokana na historia yao tangu walipoanza kuonekana pamoja mwaka 2021.
Picha na matukio yao ya pamoja yaliwafanya wengi kuamini walikuwa wameamua kuupa nafasi nyingine uhusiano wao.
Lakini kadri muda ulivyopita, maswali yameanza kurejea ikiwa safari hii wataweza kudumu au wataingia tena kwenye mzunguko wa kuachana na kurudiana.
WADAU SASA
Kadri mjadala unavyoendelea, baadhi ya watu wanaodai kuwa karibu na wawili hao wanasema wamechoshwa na hali hiyo.
Kwa mujibu wa madai yanayosambaa, baadhi yao wanaamini ni bora kila mmoja akaendelea na maisha yake kuliko kuendelea kupitia migogoro inayorejea mara kwa mara.
Wapo wanaosema wanawatakia mema wote wawili, lakini hawapendi kuona kila baada ya muda uhusiano wao ukirejea tena kwenye vichwa vya habari kutokana na sintofahamu zinazojirudia.
KAULI YA HARMONIZE YAZUA JAMBO
Hivi karibuni Harmonize alitoa kauli iliyozua mjadala alipokuwa jukwaani, akisema wakati mwingine hajisikii kuheshimiwa ipasavyo ndani ya uhusiano wake.
Msanii huyo alidai tofauti ya umri inaweza kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia changamoto hizo.
Kauli hiyo ilitafsiriwa kwa njia mbalimbali na mashabiki, huku wengine wakihusisha na hali ya sasa ya uhusiano wao.
NI NANI ANAYEPIGANIA PENZI?
Mjadala mwingine unaoendelea mitandaoni ni kuhusu nani anayejitahidi zaidi kuudumisha uhusiano huo.
Wapo wanaoamini Harmonize ndiye anayekuwa mstari wa mbele kuupigania, huku wengine wakisema Kajala pia amekuwa na mchango mkubwa katika kuufufua kila unapoyumba.
Hata hivyo, hakuna ushahidi wa wazi unaothibitisha madai hayo zaidi ya mitazamo ya mashabiki na wadau wa burudani.
WAMECHOKA?
Tofauti na zamani ambapo taarifa za wawili hao kurudiana zilikuwa zikishangiliwa, safari hii baadhi ya mashabiki wameonekana kubadili msimamo.
Wengine wanasema kama kweli wameachana tena, basi iwe mwisho wa mzunguko huo kwa sababu wamechoshwa na habari za kuachana na kurudiana kila baada ya muda.