
Julai 5, 2026, lilitokea tukio la kuhuzunisha ambapo maduka zaidi ya 54 yaliteketea kwa moto na mengine 23 kuokolewa katika eneo la Lumumba jijini Mwanza.
Janga hili la usiku wa manane liliacha vilio na simanzi kubwa kwa wafanyabiashara waliopoteza mali za mamilioni ya shilingi baada ya miundombinu yao ya kiuchumi kusambaratika ndani ya muda mfupi. Tukio hili si la kwanza kwani limekuja kufuatia mfululizo wa matukio mengine makubwa ya namna hii nchini.
Septemba 23, 2024, hukohuko Mwanza, Soko la Machinga la Ukwaju lililopo Igoma liliteketea kwa moto uliosababishwa na vijana waliokuwa wakirina asali karibu na kibanda kilichokuwa na nyuki, janga lililoathiri vibanda zaidi ya 3,000 na wafanyabiashara 70.
Tukirudi nyuma kidogo, Machi 2021, Soko la Karume jijini Dar es Salaam nalo liliteketea kwa moto wa usiku uliosababishwa na hitilafu ya umeme, na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni.
Majanga haya ya moto yanayoripotiwa mara kwa mara, yanazua hofu kubwa juu ya usalama wa kibinadamu, mali, na majengo ya umma, na yanatutaka sasa tuweke mifumo thabiti ya kinga dhidi ya moto katika masoko na majengo yote ya umma nchini.
Mara nyingi majanga ya moto masokoni na madukani hutokea nyakati za usiku, muda ambao wafanyabiashara hawapo maeneo yao ya kazi, jambo linalofanya moto kuwa mkubwa kabla ya kugundulika na kusababisha udhibiti kuwa mgumu.
Uwepo wa mifumo ya kiotomatiki ya ugunduzi na udhibiti wa moto unaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara haya ya kibinadamu na upotevu wa mali, kwani mara nyingi vikosi vya uokoaji vinapofika vinakuta uharibifu mkubwa umeshafanyika.
Ili kuweza kukabiliana na changamoto hii, kunahitajika elimu ya vitendo kwa wananchi wakiwemo wafanyabiashara masokoni, wenye maduka, na wafanyakazi ofisini ili kuepuka hasara na maafa yanayoweza kuepukika ikiwa hatua za awali zitachukuliwa kwa usahihi.
Elimu hii inapaswa kutolewa kuanzia ngazi ya serikali za mitaa sambamba na kuhamasisha kila kaya na duka kutundika mtungi wa kuzimia moto ndani, kwani linapotokea janga si wengi wenye uelewa wa kukabiliana nalo.
Ili kufikia lengo hilo kwa ufasaha, jamii ipatiwe elimu ya kujua vyanzo mbalimbali vya moto na aina ya mtungi unaotakiwa kutumika kuzimia, kwa sababu kitaalamu kuna aina tano tofauti za mitungi ya kuzimia moto na ni hatari kubwa kutumia mtungi usio sahihi.
Watu wengi huweka fikra kuwa kila aina ya chanzo cha moto kinaweza kudhibitiwa na mtungi ule uliozoeleka kuonekana kwenye kuta za maduka na ofisi, bali kitaalamu moto unaozuka kutokana na hitilafu ya umeme, kwa mfano, unapaswa kuzimwa na mtungi wenye gesi ukaa na si mtungi wa maji au povu.
Baadhi ya nyakati inashuhudiwa kutolewa kwa mafunzo ya uzimaji moto kwa kutumia mtungi wenye unga mkavu kwenye shule au maadhimisho ya sikukuu za kitaifa, jambo ambalo halikidhi umuhimu wa jamii pana kupata elimu hii adhimu.
Mafunzo hayo mara nyingi yanatafsiriwa kama igizo la muda ambapo ni watu wachache mno hupata elimu hiyo huku wengi wakikosa, jambo linalozitaka taasisi zinazofanya hivyo kubadilisha mbinu na kwenda moja kwa moja masokoni na mitaani badala ya kusubiri sherehe na maadhimisho ya kitaifa mara moja kwa mwaka.
Katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia, matumizi ya vifaa vya kielektroniki vimekuwa jambo la kawaida ofisini na masokoni, jambo linaloongeza vihatarishi vya moto na hivyo kuhitaji uwepo wa vifaa madhubuti vya kinga ya moto maeneo hayo.
Viongozi wa masoko wanapaswa kuiomba Serikali kuweka vifaa vya kukabiliana na majanga ya moto masokoni na ofisi za umma kama huduma kwa jamii, kwani wengi hushindwa kuweka mitungi hiyo kutokana na gharama kubwa ya kuinunua na kuijaza unga mkavu upya kila unapoisha muda wake wa matumizi hata ikiwa haujatumika.
Sambamba na hilo, viongozi wa masoko nchini wanapaswa kuwa na mkakati wa makusudi ambapo kila mwenye kizimba cha biashara awekewe sharti la kuwa na cheti cha kuhitimu mafunzo ya uzimaji moto kutoka Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kabla ya kupewa leseni ya biashara.
Kushitadi kwa matukio haya kunawajibisha wasimamizi wa masoko nchini kuweka utaratibu wa kufanya vikao vya mara kwa mara na wafanyabiashara, viongozi, na wataalamu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji pamoja na sekta ya afya, ili kukumbushana mikakati ya usalama wa soko.
Masoko mengi nchini pia yanakabiliwa na changamoto za uchakavu wa miundombinu kama ya maji taka, hivyo kuwepo kwa utaratibu huo wa vikao vya pamoja kunaweza kuchochea ufumbuzi wa kudumu wa mbinu za kukabiliana na majanga ya moto na kulinda mabilioni ya fedha za wafanyabiashara wetu na hata kuokoa maisha ya wananchi nchini.
Salim Mohammed ni mchangiaji wa Mwananchi mkoani Tanga.