
Dar es Salaam. “Nikiwa na umri wa miaka mitatu hiyo ilikuwa mwaka 1997 tangu kuzaliwa kwangu, nilianza kupata changamoto ya kupungua uzito kupita kiasi, kuhisi uchovu, kiu na kwenda haja ndogo mara kwa mara.
“Dalili hizo ziliwatia hofu wazazi pamoja na ndugu wa karibu na kuona haja ya kunipeleka hospitali ili kubaini chanzo cha tatizo,” anasema George Kwayu ambaye anajua vema chungu na tamu ya kuishi na ugonjwa wa kisukari aina ya kwanza kwa takribani miaka 27 sasa.
Kisukari ni ugonjwa ambao viwango vya sukari kwenye damu ya mtu au glukosi huwa vya juu kupita kiasi. Hali hii hutokea pale mwili unaposhindwa kudhibiti sukari kwenye damu inavyostahili, ambapo kwa lugha nyepesi, mfumo wa kinga ya mwili hushambulia na kuangamiza seli zinazozalisha insulini katika kongosho.
Huu ni ugonjwa ulio kwenye kundi la magonjwa yasiyoambukiza, lakini athari zake kiuchumi na kijamii ni mtihani mzito.
Kwayu ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wanaoishi na kisukari aina ya kwanza nchini Tanzania (TDYA), anaweka bayana mzigo wa matibabu unaowakabili wagonjwa wa kisukari, hasa cha aina ya kwanza.
Kwake mzigo huo anasema ni mkubwa mno na unaziacha familia nyingi zikielemewa kwa madeni. Anasema baada ya kupelekwa katika hospitali moja iliyoko mkoani Kilimanjaro na kufanyiwa vipimo, majibu yalionyesha ana kisukari aina ya kwanza.
Majibu hayo yaliwashangaza sana wazazi pamoja na ndugu waliosikia habari hiyo, huku wakitafakari imekuaje mtoto mdogo kupata ugonjwa ambao wamezoea kuusikia kwa watu wenye umri mkubwa.
Kwayu anabainisha kuwa mwanzoni taarifa hizo zilikuwa kama mwiba usiotaminika kwenye familia, ambapo baadhi walihusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina na wengine kuhisi amevamiwa na mapepo yanayohitaji maombezi ya haraka.
Wakati sintofahamu hiyo ikiendelea, wazazi wa Kwayu walishikilia matibabu na mahudhurio ya kliniki yaliyompa unafuu, na kadri siku zilivyosogea, familia ilianza kupata mwanga wa elimu kuhusu ugonjwa huo.
Safari ya maumivu
Katika safari hii ya msalaba wa maumivu, kijana huyu ambaye ni mtaalamu wa masuala ya Tehama, anasema moja ya nyakati ngumu zaidi ilikuwa ni pale mama yake mzazi alipolazimika kuuza baadhi ya mali za familia ikiwemo mifugo ili kupata fedha za kununua sindano za insulini.
Maisha yalipozidi kuwa magumu, shangazi yake aliyekuwa akiishi Dar es Salaam alilazimika kumchukua ili kumpunguzia mzigo mama yake. Alipofikisha umri wa miaka 10, msongo wa mawazo na kuchomwa sindano mara kwa mara kulimfanya akate tamaa ya kuishi, huku akilazimika kukatisha masomo na kurudishwa nyumbani kila mara afya yake ilipoyeyuka.
Ahueni na mwanga wa matumaini vilirejea baada ya kufika jijini Dar es Salaam na kuanza kliniki maalum ya watoto wenye kisukari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kwayu anasimulia kuwa alivyoona watoto takribani 30 pale, aligundua kuwa hakuwa peke yake kwenye tanuru hilo la moto, jambo lililobadilisha kabisa mtizamo na fikra zake.
Hata hivyo, ukuta mkubwa unabaki kwenye gharama. Kwayu anatolea mfano kuwa chupa ndogo ya dawa inauzwa kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000 na mgonjwa anaweza kutumia chupa mbili hadi tatu kwa mwezi kulingana na maelekezo ya daktari.
Hii ina maana mgonjwa anahitaji angalau Sh100,000 kwa mwezi kwa ajili ya dawa tu, gharama ambayo ni mlima mrefu kwa kijana anayetoka familia duni asiye na bima ya afya.
Kwayu anaenda mbali zaidi na kusema kwa aina ya insulini anayotumia yeye, analazimika kujichoma mara tatu kwa siku kulingana na mlo, ambapo chupa moja nchini inauzwa takribani Sh90,000 na inamdumu kwa siku tatu tu, achilia mbali ile anayochoma usiku.
Kwa ujumla wake, kijana huyu anajikuta akiteketeza zaidi ya Sh1.2 milioni kwa mwezi, sawa na Sh17 milioni hadi Sh18 milioni kwa mwaka ili tu kuweka mwili wake sawa.
Somo kwa jamii
Hali anayopitia Kwayu leo hii, wapo wengine kwenye jamii kwa kujua au kutojua wanaitafuta kwa udi na uvumba.
Mitindo mibovu ya maisha na kutojali ushauri wa wataalamu wa afya na lishe, unaweka watu wengi hatarini kuugua ugonjwa huu ambao kimsingi unaweza kuzuilika.
Profesa Andrew Swai, Mwenyekiti wa Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), anafichua siri kuwa ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu ni kama pete na kidole, na zaidi ya nusu ya wagonjwa wa kisukari wanasumbuliwa pia na shinikizo la damu.
Anasema ndugu hawa wawili husababishwa na ulaji usiofaa, unywaji wa pombe uliopitiliza, matumizi ya tumbaku, kutofanya mazoezi, ukosefu wa usingizi, na msongo mkubwa wa mawazo.
Kitakwimu, hali inatisha. Profesa Swai anasema miaka ya 1980, ni mtu mmoja tu kati ya 100 alikuwa na kisukari, lakini sasa idadi hiyo imepaa hadi watu 10 kwa kila watu 100.
Kimataifa, utafiti mpya uliochapishwa kwenye jarida la afya la The Lancet ukishirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO) unakadiria kuwa watu milioni 800 wanaugua kisukari duniani, likiwa ni ongezeko la zaidi ya mara nne tangu mwaka 1990.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa mwaka 2022 kulikuwa na watu wazima milioni 828 wenye kisukari duniani, huku asilimia 59 kati yao, sawa na watu milioni 445 wenye umri wa miaka 30 na kuendelea, wakiwa hawapati matibabu yoyote.
Ongezeko hili limeonekana zaidi katika nchi za kipato cha chini na kati ambapo kiwango kimeongezeka maradufu kutoka asilimia saba hadi 14 tangu mwaka 1990.
WHO inaonesha kuwa tangu mwaka 2012, ugonjwa huu ulikuwa ukisababisha vifo vya watu milioni 1.5, huku matatizo yanayotokana na sukari ya juu yakiondoa maisha ya watu milioni 2.2 kwa mwaka huo.
Wataalamu wa lishe wanasema hali hii inachangiwa na mitindo mibaya ya maisha na ukosefu wa mazoezi. Kwa upande wa Tanzania, mzigo huu ni mzito kwani ripoti ya hivi karibuni ya Wizara ya Afya ya mwaka 2025/2026, inaonyesha kuwa Watanzania 646,474 wanakabiliwa na ugonjwa huu kwa sasa.
Mbinu kukabili kisukari
Wataalamu wa afya na lishe akiwamo Ofisa mtafiti mwandamizi wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Adeline Munuo, wanataja njia mbalimbali za kukabiliana na kisukari.
Kwa mfano, wanasisitiza jamii kutumia zaidi vyakula vya mimea kama nafaka zisizokobolewa, jamii ya kunde, matunda na mboga mboga, kuliko vyakula vya wanyama.
Wanashauri matunda yaliwe yakiwa mazima badala ya kusagwa kuwa juisi, kwani juisi hufyonzwa haraka na kusababisha sukari kupanda ghafla.
Kuhusu mapishi, wanashauri kutumia mafuta kidogo yasiyozidi ukubwa wa kidole gumba kwa mlo mmoja, kuepuka nyama zenye mafuta na kutumia mafuta ya mimea.
Pia matumizi ya chumvi yasizidi kijiko kimoja cha chai kwa siku, na sukari isizidi vijiko vitano.
Wanashauri pia kuepuka vyakula vilivyosindikwa, kuacha au kupunguza pombe ambapo kwa mwanamke asizidishe chupa moja au glasi moja ya mvinyo au toti mbili za vinywaji vikali, na mwanaume asizidishe mara mbili ya kiwango hicho.
Aidha, jamii inatakiwa kuepuka vyakula vilivyoota ukungu, kuacha tumbaku, kudhibiti unene, na kuushughulisha mwili hadi utoke jasho, huku wakisisitiza mtu asikae zaidi ya saa moja bila kusimama au kujinyoosha kwa dakika mbili.
Mbinu nyingine ni kujirekebisha kisaikolojia kwa kupata usingizi wa saa saba, kudhibiti hasira na chuki, kupata chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake, na kufanya uchunguzi wa afya angalau mara moja kwa mwaka.
Munuo anamalizia kwa kuonya tabia ya kula milo mizito usiku wa manane kuanzia saa tatu au nne kisha kwenda kulala, akisema hiyo ni hatari kwa afya.