Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaack Mwakisu, amewataka wakazi wanaoishi ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Mkuti katika maeneo ya Lugufu Relini na Kacheli kuendelea kuhama kwa hiari, akisisitiza kuwa Serikali imekamilisha maandalizi ya maeneo mapya ya makazi pamoja na huduma muhimu za kijamii.
Akizungumza leo Julai 24, 2026, wakati wa ziara ya kutembelea maeneo hayo akiwa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya na wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Kanali Mwakisu amesema lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea mwitikio wa wananchi wanaotekeleza zoezi la kuhama kwa hiari.
Amesema Serikali tayari imewaandalia wananchi maeneo ya kujenga pamoja na miundombinu muhimu ikiwemo shule, ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata elimu na wananchi wanapata huduma muhimu katika makazi mapya.
Kanali Mwakisu amesema ziara hiyo inalenga pia kuhakikisha wananchi wanaelewa umuhimu wa kuhama kwa hiari na kushirikiana na Serikali katika kulinda hifadhi za misitu.
Ziara hiyo imefuatia ile ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, aliyofanya Juni 20, 2026, ambapo alihamasisha wananchi wanaoishi ndani ya maeneo hayo ya hifadhi kuhama kwa hiari ifikapo mwisho wa mwezi Julai.
(Feed generated with FetchRSS)