
Dar es Salaam. Kukosekana kwa sheria mahususi inayowatia hatiani wanaojihusisha na biashara ya ukahaba, maarufu ‘dada poa’, ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Serikali na wadau katika juhudi za kudhibiti vitendo hivyo nchini.
Sheria za Tanzania hazitambui moja kwa moja uzinzi, uasherati na ukahaba kama kosa la jinai, bali hulichukulia zaidi kama suala la maadili.
Kutokana na hali hiyo, wataalamu wa sheria wanasema mamlaka za Tanzania hukabiliwa na ugumu wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika, hata wakienda mahakamani ni sawa na bure ikiwa hakutakuwa na mabadiliko ya sheria.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, sheria zilizopo hazielezi kwa uwazi mazingira yanayofanya ukahaba kuwa kosa la jinai ili mtu afikishwe mahakamani na kutiwa hatiani,hivyo ni lazima zitungwe zinazotamke bayana kuwa kitendo hicho ni kosa.
Mbali na sheria, ugumu mwingine hutokana na namna vitendo vyenyewe vinavyobadilika kulingana na mazingira ya kijamii, kiuchumi na maendeleo ya teknolojia.
Katika miji mikubwa nchini, biashara hiyo imekuwa ikibadilika kutoka kwenye maeneo ya wazi kama mitaa maarufu, baa na maeneo ya starehe, na kuhamia zaidi kwenye matumizi ya mitandao ya kijamii, programu za mawasiliano na majukwaa ya mtandaoni yanayorahisisha wahusika kuwasiliana kwa siri.
Tanzania imejikuta kwenye mtihani mgumu, kwa mamlaka mbalimbali nchini kufanya operesheni katika maeneo yanayotajwa hufanyika biashara hizo, ingawa hufanyika kwa muda mfupi na hali kurejea tena.
Msingi wa hoja za wadau unatokana na mjadala wa kitaifa baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, hivi karibuni kudai ili operesheni zinazofanyika maeneo mbalimbali kudhibiti biashara hiyo hazipaswi kuwaangalia wanaouza huduma hiyo pekee, bali pia wanaionunua.
Wakizungumza na Mwananchi, wadau wa sheria wanasema ukahaba ni suala linaloangukia kwenye kosa la kimaadili, hivyo linapaswa kushughulikiwa kwa mtindo huo lbadala ya kwenda mahakamani ambako huwezi kufanikiwa.
Wakili Peter Madeleka amesema kuwa mwaka 2024 aliwahi kuendesha kesi ya kutetea wanawake ‘madada poa’ waliokamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya ukahaba katika Wilaya ya Ubungo.
Amesema baada ya watuhumiwa hao kufikishwa mahakamani, Serikali iliiacha kesi hiyo ikiendelea mahakamani kwa madai kuwa ilikuwa inaenda kuomba rejea.
Madeleka amesema kwa mtazamo wa kisheria, ukahaba si kosa linalotambuliwa na sheria za Tanzania na kauli zinazotolewa na waziri kuhusu suala hilo ni mwendelezo wa siasa badala ya hoja za kisheria.
“Ndiyo maana tunaona miaka nenda rudi jambo hili limeendelea kuwepo kwenye jamii, kwa sababu sheria imeshindwa kueleza ni kwa namna gani tabia hizo zinakuwa kosa. Ili mtu afikishwe mahakamani ni lazima sheria itamke wazi kuwa kitendo hicho ni kosa,” amesema.
Amesema kuzungumzia suala hilo kwenye majukwaa ya kisiasa na kuwapa watu majina, ilhali sheria haisemi hivyo, kunaweza kusababisha aliyetoa tuhuma kujidhalilisha pindi suala hilo linapofikishwa mahakamani.
“Siamini anachokisema waziri kama kina msingi katika jicho la kisheria,” amesema.
Madeleka amesema suala la ukahaba linahusu zaidi maadili kuliko jinai, sawa na vile mtoto kushindwa kumsalimia au kumwamkia mtu mzima.
“Kutokumpisha kiti akae mtu aliyekuzidi umri si kosa la kisheria bali ni kosa la kimaadili. Kwa hiyo, mambo haya ya kimaadili yanapaswa kushughulikiwa kwa misingi ya maadili,” amesema.
Amesema, kwa kuwa kuna wizara inayohusika na masuala hayo, ni muhimu kutoa elimu kupitia nyumba za ibada na taasisi nyingine za kijamii, ili kusaidia kukomesha biashara ya ukahaba.
“Sidhani kama hapa tulipofika ukahaba ndio unaofanya Tanzania isipige hatua za maendeleo. Kuna makosa mengine, kama wizi, ambayo ni makosa ya kimaadili na kisheria, lakini huoni Serikali ikiweka nguvu za aina hiyo kuyatokomeza,” amesema.
Mtazamo wa Madeleka unaungwa mkono na Wakili Onesmo Kyauke, pia akisema ni vigumu kudhibiti biashara hiyo kutokana na mabadiliko ya namna wahusika wanavyowasiliana, akisisitiza kwa sasa wanatumia zaidi mitandao ya kijamii.
“Binafsi nimeishi Kinondoni kwa muda mrefu. Zamani ilikuwa ni jambo la kawaida kuwaona wakisimama barabarani wakijiuza, lakini siku hizi hawaonekani. Wengi wamehamia mitandaoni, ambako wanawasiliana na kupanga sehemu za kukutana,” amesema.
Kyauke amesema vitendo hivyo hufanyika kwa usiri mkubwa, baadhi ya mataifa yaliwahi kupambana kuvimaliza lakini yalishindwa, na baadaye yalilazimika kuvirasimisha na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya shughuli hizo.
“Kama tunataka kukomesha tatizo hili, jambo la msingi ni kutoa elimu ya maadili kwa wahusika. Pia, kama chanzo ni ukosefu wa ajira kwa wanawake, basi waangaliwe kwa jicho la tofauti na kusaidiwa. Wapo wanaojiuza kutokana na umaskini, lakini pia wapo wenye uwezo mkubwa kifedha wanajiuza,” amesema.
Amesema kuwafikisha wahusika mahakamani si jambo rahisi kutokana na ugumu wa kupata ushahidi wa kutosha wa kuwakamata.
“Hata Jeshi la Polisi likiwakamata, mara nyingi huachiliwa baadaye,” amesema.
Kyauke ameongeza: “Ni muhimu kuwasaidia na ikiwezekana ufanyike utafiti wa kina kubaini sababu zinazowasukuma kufanya biashara hiyo. Wapo wanaoishi mitaani bila ajira, wengine ni matajiri, wengine hawana njia nyingine ya kujikimu, na wengine hupatikana katika baa,” amesema.
Kyauke pia amehoji uwezekano wa kuwawajibisha wanaume wanaonunua huduma hizo, akisema mazingira ya kisheria nchini Tanzania ni tofauti na yale ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ambako uzinzi na uasherati ni makosa ya jinai.
“Hata huyo mwanaume utamkamata kwa kosa lipi? Kwa mfano, unaweza kumtongoza mwanamke anayefanya kazi kwenye kasino na akakubali kuondoka na wewe. Kosa liko wapi?” amehoji.
“Mwanaume wa namna hiyo utamkamata kwa kosa gani? Kila mwanaume mwenye mpenzi au mke humhudumia kifedha. Kuna tofauti gani kati yake na yule anayelipa fedha kwa mwanamke anayejihusisha na biashara hiyo barabarani?” amehoji.
Mjadala wa wanasheria hao unatokana na kauli ya Waziri Katambi,ya hivi karibuni kuwa udhibiti wa biashara ya ukahaba unapaswa kujumuisha kuwakamata wanunuzi wa huduma hizo, kwa kuwa bila wao biashara hiyo isingeweza kuendelea.
Alisema suala hilo linapaswa kushughulikiwa kwa mtazamo sawa na makosa ya rushwa, ambapo anayetoa na anayepokea wote huchukuliwa hatua za kisheria, akitoa mfano kuwa aliwahi kutekeleza utaratibu huo alipokuwa mkuu wa Wilaya ya Dodoma.
“Nilikuwa nakamata madada poa, lakini niliona wanaonunua wanawasha magari yao na kuondoka. Wengi wao walikuwa watumishi wa taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi. Nilipoanza kuwakamata pia, hali ilitulia,” alisema.
Katambi si wa kwanza
Hatua anayoeleza Katambi si mara ya kwanza kuchukuliwa wa viongozi nchini, wakijaribu kukabiliana na biashara hiyo kwa operesheni maalumu, bila mafanikio ya kupigiwa mfano.
Katika nyakati tofauti, viongozi mbalimbali wameibua mikakati ya kuondoa biashara hiyo, lakini uzoefu unaonyesha kuwa imekuwa vigumu kupata suluhisho la kudumu.
Akiwa mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yuduph Makamba aliwahi kusimamia operesheni mbalimbali zilizolenga kudhibiti vitendo vinavyodaiwa kuharibu maadili katika jiji hilo, ikiwemo biashara ya ngono katika maeneo mbalimbali.
Operesheni hizo zililenga kusafisha maeneo yaliyotajwa kuwa na mkusanyiko wa wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo, lakini baada ya muda hali ilijirudia.
Baadaye, viongozi wengine wa wilaya na mkoa waliendelea kuchukua hatua katika maeneo mbalimbali bila mafanikio.
Licha ya juhudi hizo, changamoto kubwa imeendelea kuwa namna ya kuthibitisha tuhuma dhidi ya wahusika, kwani biashara hiyo mara nyingi hufanyika kwa siri, huku baadhi ya wanaokamatwa katika operesheni wakihitaji ushahidi wa kisheria ili kufikishwa katika hatua nyingine.
Ndiyo maana wataalamu wa sheria wanaeleza kuwa operesheni pekee haziwezi kumaliza tatizo kama hakuna ushahidi wa kutosha, hadi hapo sheria zitakapolitambua kosa hilo.