Mpwapwa. Serikali imesema idadi ya wananchi wanaonufaika na huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano bado ni ndogo licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa, na kulitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuongeza kasi ya kuwaunganisha wananchi, taasisi za Serikali na sekta binafsi kwenye huduma hiyo.

Agizo hilo limetolewa leo Ijumaa, Julai 24, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Mpwapwa, mkoani Dodoma ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa kwa Waziri, Mkoa wa Dodoma una watu 65 pekee waliounganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi sasa, licha ya uwekezaji mkubwa uliofanyika katika miundombinu hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Kairuki ameiagiza TTCL kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kusudi  Watanzania wengi zaidi wanufaike na fursa zinazotokana na uchumi wa kidijitali na kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Licha ya Serikali kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika ujenzi na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, bado idadi ya wananchi wanaonufaika na huduma hiyo ni ndogo. Kuna haja ya kuongeza juhudi za kuwafikia Watanzania wengi zaidi kama lengo la mradi linavyokusudia,” amesema Kairuki.

Amesema matumizi mapana ya Mkongo wa Taifa yatasaidia kupunguza gharama za mawasiliano, kuboresha huduma za Serikali mtandao, kuimarisha biashara za kidijitali na kuongeza ufanisi katika sekta muhimu zikiwamo elimu, afya na uwekezaji.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha teknolojia inakuwa kichocheo cha maendeleo na wananchi wote wanapata fursa sawa za kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Katika ziara hiyo, Waziri huyo ametembelea ofisi za TTCL na Shirika la Posta Tanzania wilayani Mpwapwa, ambako alikagua utoaji wa huduma pamoja na maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano.

Kwa mujibu wa takwimu za Serikali, Mkoa wa Dodoma una minara 488 ya mawasiliano inayohudumia zaidi ya wananchi 150,000, huku ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ukiwa umekamilika kwa urefu wa kilomita 942.5.

Kairuki amesema Wilaya ya Mpwapwa tayari ina minara 57 ya mawasiliano iliyoboreshwa, ambayo imefikisha huduma katika kata 28, huku akiahidi kuwa kata tano zilizobaki zitapatiwa huduma hiyo katika kipindi kifupi kijacho.

Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kupanua huduma za mawasiliano nchini, ikiwamo ujenzi wa minara 636 inayotarajiwa kukamilika Machi 2027, pamoja na mradi mwingine wa minara 280 utakaoongeza zaidi wigo wa huduma.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Serikali inaendelea kuboresha huduma muhimu kwa wananchi, ikiwamo upatikanaji wa maji safi na salama kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo tofauti ya mkoa huo.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uchimbaji wa visima viwili katika vijiji vya Tambi na Mlembule, pamoja na mradi wa maji wa Kijiji cha Wiyenzele unaotekelezwa kwa ushirikiano na wadau wa Water for People, wenye thamani ya Sh891 milioni.

Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Dodoma, Simon Marwa amesema hatua ya awali ya mradi wa Mkongo wa Taifa ilikuwa kuunganisha ofisi za Serikali na taasisi za umma, huku hatua inayofuata ikiwa ni kuwafikia wananchi binafsi ili kuongeza matumizi ya huduma hiyo.

Mkazi wa Kijiji cha Mlembule, Japhet Rafael amesema huduma za mawasiliano zimekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi, hasa katika biashara za mtandaoni na kurahisisha mawasiliano.

Kwa sasa tunatumia mtandao kufanya biashara mtandaoni na kuwasiliana kwa urahisi na ndugu zetu. Tunaipongeza Serikali kwa hatua hii ambayo imetuwezesha kufaidika na huduma kama ilivyo kwa wananchi wa mijini,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *