Dar es Salaam. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) imetaja ukosefu wa elimu kwa baadhi ya madereva kuhusu usafirishaji wa kemikali hatarishi, pamoja na kutotambua aina ya mizigo wanayosafirisha, kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia ajali zinazohusisha kemikali hizo.

Mamlaka hiyo imesema hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya madereva kumwaga kemikali barabarani wanapopata ajali au hitilafu nyingine, jambo linalohatarisha usalama wa wananchi na mazingira.

Kauli hiyo inakuja wakati ajali nyingine iliyohusisha lori lililokuwa likisafirisha kemikali aina ya sulphurikitokea alfajiri ya leo, Ijumaa, Julai 24, 2026, katika eneo la Mafiga, mkoani Morogoro.

Katika ajali hiyo, mtu mmoja amefariki dunia na wengine wawili kujeruhiwa baada ya lori lililokuwa limebeba kemikali hiyo kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa likisafirisha mchanga.

Baada ya kugongana, lori la mchanga lilishika moto na kuteketea.

Ajali hii inatokea takribani miezi miwili tangu kutokea ajali nyingine iliyohusisha lori lililokuwa likisafirisha kemikali hiyo katika eneo la Mindu, kwenye barabara hiyo, hali inayoendelea kuibua wasiwasi kuhusu usalama wa usafirishaji wa kemikali na magari makubwa yanayotumia njia hiyo.

Licha ya sheria ya GCLA kuwalazimisha wasafirishaji kuwatumia madereva wenye mafunzo ya usafirishaji wa kemikali hiyo, wasafirishaji wamesema baadhi ya kampuni huwapeleka madereva wachache kupata mafunzo na wengine hubaki bila mafunzo, na ndio wamekuwa wakipata ajali.

Ili kukomesha ajali hizo, wasafirishaji wameazimia GCLA isiruhusu usafirishaji wa kemikali hiyo usiku na mwisho wa kusafirisha uwe saa 12 jioni. Pia, msafirishaji anayehusika na ajali nyingi aondolewe kwenye mfumo wa usafirishaji.

Pia wamependekeza kuwadhibiti waingizaji wa kemikali ambao ndio watakaosimamia kampuni zinazosafirisha ziwe na madereva wenye mafunzo, na kampuni zizingatie usalama wa mnyororo mzima wa usafirishaji.

Pia wamependekeza kiwango cha usafirishaji wa kemikali hiyo kipunguzwe kutoka tani 30 hadi 20 ili kupunguza hatari, kampuni zinazosafirisha kemikali hizo ziwe na magari ya kusindikiza magari yanayosafirisha kemikali, na GCLA ifanye tathmini ya kampuni zenye ajali nyingi na kuzichukulia hatua kali.

Mapendekezo hayo yanakuja ikiwa ni siku chache tangu Julai 20, 2026, gazeti la Mwananchi kuonyesha hatari inayowakumba madereva wanaosafirisha kemikali hiyo, ambao wengine hupoteza maisha au kupata maradhi kutokana na kutokuzingatiwa kwa usalama wa usafirishaji wa kemikali hiyo.

Takwimu za GCLA zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2024 na 2026 kumekuwa na ajali 62 zinazohusisha usafirishaji wa sulphur, huku ajali nyingi zikitokea mkoani Morogoro.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, akizungumza leo Ijumaa, Julai 24, 2026, jijini Dar es Salaam na wahifadhi, wasafirishaji na waagizaji kuhusu namna ya kuimarisha usalama wa kemikali hiyo, amesema tangu Julai 2021 hadi sasa, kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga, jumla ya meli 112 zimeingiza zaidi ya tani milioni 3.74 za salfa nchini.

“Takwimu zinaonyesha kati ya mwaka 2024 na 2026 kumekuwa na ajali 62 zinazohusisha usafirishaji wa sulphur. Ingawa idadi hiyo inaweza kuonekana ndogo ukilinganisha na kiasi kikubwa cha mizigo inayosafirishwa, hata ajali moja inaweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu, mazingira na miundombinu,” amesema.

Ndiyo amesema baadhi ya ajali zimesababisha kumwagika kwa kemikali barabarani, nyingine zimehusisha reli, na zingine zimehatarisha vyanzo vya maji au kusababisha hatari ya moto.

Kwa upande wake, Meneja wa GCLA Kanda ya Kati, Magdalena Mtenga, amesema kiwango cha ajali sasa ni kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo katika kanda yake pekee ajali 17 zimetokea katika mwaka 2025/26.

Amesema baadhi ya ajali hutokea madereva wanapomwaga kemikali ya sulphur kabla ya kufika Hifadhi ya Mikumi na hata baada ya kuipita hifadhi hiyo, akihoji kwa nini hali hiyo hutokea.

“Tumeangalia kwa nini ajali ni nyingi. Madereva hawana mafunzo, wanapewa mizigo tu wanasafirisha, hawana vifaa vya usalama (PPE), kampuni hazina mipango ya dharura.

“Inapotokea ajali hadi sisi tena ndio tutoke tukaondoe kemikali husika barabarani. Sheria inataka kampuni iwe na watu wake wa kushughulikia changamoto ya ajali inapotokea,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa GCLA Nyanda za Juu Kusini, Elias Mulima, amesema katika mwaka 2024/26 katika kanda hiyo ajali 24 zimetokea.

“Ili kudhibiti hali hii ni lazima madereva wapewe mafunzo ya kile walichobeba, magari ya kusafirisha kemikali yawe na ubora na madereva waongeze umakini wanaposafirisha kemikali,” amesema.

Mwakilishi wa Kampuni ya Mainland, Francisco Mazigo, amependekeza kampuni zinazoingiza kemikali hizo ndizo zianze kudhibitiwa kwa kuhakikisha zinatumia kampuni za usafirishaji zinazofuata sheria.

Amependekeza kuwe na ukaguzi wa kemikali hiyo katika maeneo ya kupakia, na GCLA iwaadhibu waingizaji wa kemikali wanaochukua wasafirishaji wasio na sifa.

George Alando wa Kampuni ya Uhifadhi wa Kemikali Dar es Salaam Corridor Group (DCG) amependekeza kampuni zibanwe na GCLA ziache kuchukua kila aina ya dereva kusafirisha kemikali za sulphur.

“Kuwe na mafunzo ya ndani ya kampuni husika ili kuwajengea uwezo madereva, kuwa na mifumo ya kisasa ambayo itakuwa inamfuatilia dereva akiwa barabarani kuangalia tabia yake, kwa kuwa baadhi ya madereva tabia hubadilika wakiwa njiani,” amesema.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kampuni ya Usafirishaji wa Mizigo ya TransCargo Limited, Agnes Mahenge, amesema hakuna dereva anayeruhusiwa kulala kwenye gari wakati wa kusafirisha kemikali.

Amesema kulingana na maelekezo yao kwa madereva, kila baada ya saa nane wanapaswa kupumzika, lakini wengine hawafuati utaratibu huo na hao ndio hutoka katika kampuni ambazo hazitoi elimu kwa madereva hao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *