Mwanza. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeziandikia barua taasisi za kimataifa, likiwemo Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (Amnesty International), Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), kuwaelezea kuhusu tuhuma za ugaidi zinazoendelea dhidi ya makada wao na vijana wanaoshtakiwa mahakamani.
Akizungumza leo Jumamosi, Julai 25, 2026 na waandishi wa habari katika Ofisi ya Kanda ya Victoria ya chama hicho jijini Mwanza, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche amesema tayari barua zimeandaliwa tangu Julai 24, 2026 na zitafika katika ofisi hizo Jumatatu, Julai 27, 2026.
Amesema hatua hiyo ni kuionyesha dunia kuhusu kile alichokiita mwendelezo wa makada wa chama hicho na watu wanaoikosoa Serikali kubambikiwa kesi.
Amesema ndani ya wiki mbili, zaidi ya viongozi 51 wa chama hicho wamekamatwa na kushtakiwa kwa tuhuma za ugaidi, akiwemo Katibu wa Chadema Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami.
“Tutawaandikia Amnesty International, tutaandikia UN Human Rights Council (Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa)… Tutaandikia kila mtu. Tumedraft barua kuanzia jana (Julai 24, 2026), kwa hiyo barua nyingi zimeshadraftiwa na kuanzia Jumatatu (Julai 27, 2026) zitakuwa kwenye ofisi zinazohusika,” amesema.
Mke wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibungilo A, Fantson Mpango ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wa ugaidi, Elizabeth Richard akizungumza kwenye mkutano kati ya waandishi wa habari na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche. Picha na Saada Amir
Ameongeza kuwa: “Tunaandika barua na tunafanya hivyo ili dunia ijue. Siyo CAF tu na Fifa… tutaandikia mashirika yote ya kimataifa kwamba kuna wanachama wetu 51, kwa mujibu wa Serikali ya Samia, wameshtakiwa kwa kesi ya ugaidi. UN mtusaidie na watu wajue.
“Hili jambo likienda kimya kimya linatuumiza sisi… na mtu anayesema sisi tunachafua nchi kimataifa ni mjinga kabisa… tutawaambia kila mtu, Umoja wa Ulaya, Marekani, tutawaambia.”
Amesema wanaochafua nchi kimataifa ni wanaofanya matukio ya utekaji, kuua na kubambikia watu kesi, na kwamba hawatakaa kimya bali watapaza sauti kuomba msaada duniani na kwa majirani.
“Nchi kama hii ambayo imepoteza leadership haiwezi kuendelea, inatishia hata maendeleo ya utalii na uwekezaji kwa kuwa hakuna atakayewekeza au kuja nchini kutalii… wageni hawawezi kuja kwenye nchi inayosemekana kuna ugaidi.
“Nani atakwenda kwenye kiwanja akakae kwa amani wakati kuna ugaidi… Kitendo cha kutangaza kuna ugaidi wakati ni uongo ni kitendo cha hatari kinachochafua nchi,” amesema.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 25, 2026 katika ofisi ya Kanda ya Victoria ya chama hicho. Picha na Saada Amir
Amesema: “Tunaomba TLS kupitia Section 4, wanajua kazi ya TLS ni kulinda watu wanaoonewa… LHRC (Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu) watusaidie, watetezi wa haki za binadamu na mashirika ya kimataifa watusaidie kutuongezea nguvu, kutusaidia fedha za kuwaongezea mawakili ili wafanye kazi.”
Amewashukuru Watanzania akisema kila siku wanawachangia zaidi ya Sh15.5 milioni, akitaka waendelee kuongeza nguvu za mawakili kushughulikia watuhumiwa wa ugaidi.
Amesema wamekuwa wakifuatilia kesi ya Tundu Lissu tangu mwaka jana, huku kesi hiyo ikisimama, akidai ni mtu anayepaswa kushindana kisiasa lakini ameonewa.
“Tunafikiri ofisi ya DPP ni ofisi inayopaswa kufumuliwa na kuundwa upya, ndiyo maana tunataka Katiba mpya,” amesema.
Amesema: “Siku ya Sheria Samia alisema wanaharakati ni magaidi. Baada ya hapo watu 51 ndani ya wiki mbili wamepewa kesi za ugaidi. Kwa hiyo ni njama ya kuumiza viongozi wanaompinga ambao wapo kwa mujibu wa sheria.”
Katika hatua nyingine, Heche amewatahadharisha wahadhiri wanaoendelea kufundisha darasani wakati mwenzao amebambikiwa kesi ya ugaidi, akisema hakuna aliye salama na kwamba sauti lazima zipazwe.
Hofu ya kupewa kesi ya ugaidi
Heche ameonyesha hofu ya huenda na yeye akabambikiziwa kesi ya ugaidi kwa mara nyingine, akidai kuwa kuna dalili zinazoonyesha analengwa kutokana na nafasi yake ndani ya chama.
Amesema uwezekano huo unatokana na madai ya vijana wa Chadema mkoani Mbeya ambao anasema waliamrishwa kusema na kurekodiwa kuwa yeye ndiye aliyewatuma kufanya vitendo vya kigaidi na aliwapa Sh60 milioni.
“Kabla sijawa Makamu Mwenyekiti, sijawahi kuwa targeted (kulengwa). Nimefika hapa nimekuwa targeted… jana mmeona hata picha zinasambazwa kwamba mke wangu amekamatwa nchini Ghana, mambo mbalimbali kwa sababu nalengwa.
“Ni jinsi gani wanaweza kuchafua credibility (hadhi) yangu, ni jinsi gani wanaweza kuniweka ndani, ni jinsi gani wanaweza kunidhuru… naelewa dereva wangu recently (hivi karibuni) ameuawa katika mazingira yenye utata kabisa. Ni ujumbe kwangu, we are one step away from you (tuko hatua moja kabla ya kukufikia),” amesema.
Amesema tangu alipokuwa Njombe amekuwa akifuatiliwa na kwamba kusambazwa kwa taarifa za uongo, ikiwemo madai ya kukamatwa kwa mke wake, ni sehemu ya juhudi za kumchafua na kumdhoofisha kisiasa.
“Dalili zipo zote. Mimi nilikamatwa, nikakaa siku 21 mahabusu… nimekaa Mtumba siku 14, nikahamishiwa Mburahati siku 7 bila maelezo yoyote, kinyume na sheria,” ameeleza.
Naye, mke wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Ibungilo A, Fantson Mpango, ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wa ugaidi, Elizabeth Richard amesema mume wake alikamatwa Julai 8, 2026 akiwa kwenye kikao cha ODC, akisema hiyo ni mara ya tatu anakamatwa.
“Nina familia yenye watoto wanne… kawekwa gerezani, yeye ndiye anayefanya kazi. Mungu amsaidie atoke ili watoto wake waendelee na masomo. Tungependa arudi nyumbani ahudumie familia,” amesema.