Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu katika Ardhi za Palestina Zinazokaliwa kwa Mabavu, Francesca Albanese, ameyataja mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kuwa ni “mauaji ya kimfumo”, na kuitaka jamii ya kimataifa kuweka mara moja vikwazo vya silaha pamoja na kusitisha biashara na utawala huo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu lililonukuliwa na IRNA, Albanese aliandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba mauaji ya kimfumo dhidi ya raia wasio na ulinzi katika maeneo mbalimbali ya Ukingo wa Magharibi yanaendelea huku Ukanda wa Gaza ukiendelea kushambuliwa.

Amesema walowezi wa Kizayuni na jeshi la utawala huo wanashirikiana katika mashambulizi hayo, akisisitiza kuwa, jukumu la matukio hayo haliwezi kubebeshwa tu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu au watu wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Albanese aliongeza kuwa kuwekwa vikwazo vya silaha na kusitishwa biashara na utawala wa Kizayuni ni hatua za dharura zinazohitajika kwa mujibu wa sheria za kimataifa ili kuzuia ukiukaji zaidi wa haki za binadamu.

Mapema siku ya Ijumaa, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na waziri wa vita wa utawala huo, Israel Katz waliamuru “operesheni kubwa ya kijeshi” inayolenga miji na vijiji vya Palestina kote katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Baadaye, walowezi wa Kizayuni walishambulia vijiji vya Palestina vya Sarra na Urif katika mkoa wa Nablus, wakichoma moto nyumba na mali nyinginezo.

Wakati huo huo Wapalestina sita wameuawa na wengine 37 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel kote Gaza katika saa 48 zilizopita. Hayo ni kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza

Idadi ya vifo kutokana na uvamizi wa kijeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza imefikia 73,317, wizara hiyo ilisema siku ya Jumamosi, huku mashambulizi ya Israel katika eneo hilo yakiendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *