Rais Donald Trump wa Marekani hatimaye ametiliana saini na Saudi Arabia makubaliano ya ushirikiano wa nishati ya nyuklia kwa matumizi ya kiraia, ambayo yanafungua njia kwa ajili ya shughuli za kurutubisha urani ndani ya ufalme huo.

Kama ilivyoripotiwa na magazeti ya Wall Street Journal na New York Times, kupitia makubaliano hayo ya miaka 30, ambayo thamani yake inakadiriwa kufikia makumi ya mabilioni ya dola, Riyadh itapata fursa ya kutumia teknolojia ya nyuklia kwa “matumizi ya kiraia” kwa msaada wa Washington. Chini ya makubaliano hayo, makampuni ya Marekani yatakuwa na nafasi muhimu katika kuanzisha na kuendeleza miundombinu ya nyuklia nchini Saudi Arabia, na kuzuia makampuni mengine ya kigeni kufanya kazi katika sekta hiyo nchini humo.

Idhini ya Trump ya kuhamisha teknolojia ya nyuklia ya Marekani kwenda Saudi Arabia imevutia vyombo vya habari kimataifa. Riyadh inadai kuwa inahitajia teknolojia ya nyuklia ya Marekani ili kupunguza utegemezi wake kwa mafuta ya visukuku. Hata hivyo, makubaliano kama hayo itabidi yafuate kanuni kali za kutosambaza silaha za nyuklia na kukabiliwa na uchunguzi mkali wa bunge la Marekani. Chini ya mojawapo ya vipengele vya makubaliano hayo, iwapo utafiti wa pamoja kati ya mataifa hayo mawili utafanikiwa, kampuni za Marekani zitajenga kituo cha kurutubisha nyuklia nchini Saudi Arabia. Pamoja na hayo suala hili limekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wa vyama vikuu vyote viwili vya kisiasa nchini Marekani pamoja na watawala wa Israel, ambao wanachukulia hatua hiyo kama njia inayoweza kuiwezesha Saudi Arabia kutengeneza silaha za nyuklia.

Ni muhimu kuzingatia kuwa Marekani inadumisha msimamo wa undumakuwili kuhusiana na suala zima la teknolojia ya nyuklia katika eneo la Asia Magharibi. Ingawa Washington imekuwa ikipinga mara kwa mara Iran kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa malengo ya amani kwa madai kuwa inataka kutengeneza silaha za nyuklia, lakini wakati huo huo inaunga mkono uhamishaji wa teknolojia kwa washirika wake wa kikanda.

Licha ya ukweli kwamba makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, ya mwezi Juni 2015 kati ya Iran na kundi la 5+1, yalifikiwa kwa shabaha ya kuhakikisha shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani kupitia utekelezaji wa taratibu kali zaidi za ukaguzi wa nyenzo na vituo vyake vya nyuklia, lakini Trump alitangaza kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano hayo mwezi Mei 2018 na kisha kuweka vikwazo vikali dhidi ya Iran, kama sehemu ya kampeni ya “mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi.” Hii ni licha ya ukweli kwamba hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa Iran inataka kutengeneza silaha za nyuklia, ambapo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) tayari umesisitiza mara kwa mara kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani. Aidha, ripoti za vyombo vya kijasusi vya Marekani pia zimethibitisha kuwa Iran haijihusishi na jitihada za kutengeneza silaha za nyuklia. Hata hivyo, bila kujali ukweli huu, Trump anapinga hasa shughuli za Iran kurutubisha urani, pamoja na kuwa Iran ambayo ni mwanachama wa IAEA na Mkataba wa Kutosambaza Silaha za Nyuklia (NPT), ina haki ya kuendesha shughuli za nyuklia kwa malengo ya amani, ikiwemo urutubishaji urani.

Hatimaye, mara tu baada ya kuingia katika muhula wake wa pili, Trump aliamuru kushambuliwa kwa mabomu vituo vya nyuklia vya Iran wakati wa vita vya siku 12 mnamo Juni 2025. Muda mfupi baadaye, alitumia madai bandia ya uwepo wa tishio kwa usalama wa taifa wa Marekani kutoka kwa Iran, hasa kuhusiana na mpango wake wa nyuklia, na kuanzisha vita vya siku 40 dhidi ya nchi hii tarehe 28 Februari 2026. Ingawa Trump amesisitiza mara kwa mara kuwa aliharibu kabisa vituo vya nyuklia vya Iran, lakini ameendelea kufanya mashambulizi ya mara kwa mara ya anga na makombora dhidi ya maeneo mbalimbali nchini Iran wakati wa kipindi cha usitishaji vita na kufuatia kujiondoa kwake katika Makubaliano ya Islamabad. Wakati huo huo, Marekani inatekeleza hadharani siasa za undumakuwili kuhusiana na suala hili hili kwa kuwezesha teknolojia ya nyuklia kuwafikia washirika wake katika eneo la Asia Magharibi. Kama tulivyoashiria mwanzoni, ametia saini makubaliano ya ushirikiano wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia na Saudi Arabia ambayo yanafungua njia kwa ajili ya urutubishaji wa urani ndani ya ardhi ya nchi hiyo, huku akionyesha upinzani mkali dhidi ya shughuli yoyote ya urutubishaji wa urani inayofanywa na Iran na hata kutaka kufungwa vituo vyote vya nyuklia vya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *