Babati. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeruka kiunzi cha kwanza baada ya Mahakama kukipa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama dhidi ya Msajili wa vyama vya Siasa.

Mbali na kutoa kibali hicho, Mahakama Kuu Masjala ndogo ya Manyara, imeyatupa mapingamizi matatu yaliyokuwa yamewekwa na Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na pia imetoa zuio la muda kwa Msajili kukiadhibu Chadema.

Uamuzi huo umetolewa Julai 23, 2026 na Jaji Irvin Mgeta wakati akitoa uamuzi wa maombi namba 12812 ya 2026 yaliyofunguliwa na Katibu Mkuu Chadema na Bodi ya Wadhamini ya chama hicho dhidi ya Msajili na AG.

Awali maombi hayo ya Chadema kupitia kwa mawakili Mpare Mpoki, Nyaronyo Kicheere, Jebra Kambole na Hekima Mwasipu, yalikutana na mapingamizi ya awali kutoka kwa Msajili na AG, lakini yalipanguliwa.

Mapingamizi hayo yalihusu viapo vya waleta maombi kwamba vilikuwa na dosari za kisheria kwa kuingiza maoni, hoja, maneno ya kuambiwa na hitimisho, hivyo wakataka maombi hayo ya Chadema yatupwe, hoja zilizopanguliwa na Chadema.

Jaji Mgeta alisema mapingamizi yote matatu yanatupwa kwa kuwa hayana mashiko.

Akitoa uamuzi kuhusu maombi, Jaji alisema msingi wa maombi hayo ni barua ya Msajili wa vyama vya Siasa ya Mei 7, 2026 ikimtaka Katibu mkuu Chadema kuwasilisha utetezi wa kwa nini chama hicho kisisimamishwe au kupigwa faini.

Hii ni kutokana na kile Msajili wa Vyama vya Siasa alichodai kuwa ni chama hicho kukiuka masharti ya usajili wake, jambo ambalo limeisukumaa Chadema kuomba kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama kumzuia Msajili asichukue hatua hizo.

Katika barua hiyo, Msajili wa vyama vya siasa alidai katika kutekelezwa majukumu yake, Chadema kimekuwa kikikiuka kifungu cha 9(2) na 19(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa nchini (Sura ya 258), kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2023.

Msajili alivitaja vitendo vinavyofanywa na Chadema kuwa ni pamoja na kuingilia shauri la uhaini linalomkabili mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho, Tundu Lissu kwa kushinikiza aachiwe bila masharti, jambo ambalo linaingilia mchakato wa haki.

Jambo la pili alilodai Msajili ni kuwa viongozi wa Chadema wamekuwa wakitoa matamshi ya uchochezi na kauli ambazo ni za kutusi na kutowaheshimu viongozi akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chadema wanapinga madai hayo na wanaamini kwa barua hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, alitenda bila mantiki, bila sababu ya msingi na kinyume cha sheria.

Moja, ni kwa kutumia kifungu kinachohusu vyama vyenye usajili wa muda wakati chenyewe ni chama chenye usajili wa kudumu, pili kwa kunukuu kauli za wanachama ambazo ni za binafasi na tatu kuitaka Chadema kutoa maelezo ya kina ya utetezi.

Pia Chadema inaeleza kuwa ina wasiwasi kuwa Msajili alichukua hatua hiyo kwa kukiuka maadili na kanuni za haki asilia na kwamba kwa yaliyoyaeleza ni kama Chadema imeshahukumiwa na Msajili.

Katika kuthibitisha hilo, katika kiapo kilichoambatana na maombi hayo, Chadema wameeleza kuwa baada ya kupewa notisi, Msajili alinukuliwa na ITV akiwataka Chadema kujibu barua yake, jambo ambalo wanadai linaonyesha upendeleo.

Chama hicho kinadai kusimamishwa kwa ruzuku ya Chadema bila kufuata taratibu sahihi za kisheria, na kukataa kutambua sekretarieti ya chama na wajumbe wa kamati tendaji waliochaguliwa kihalali ni upendeleo na ukandamizaji.

Uamuzi wa Jaji

Katika uamuzi wake, Jaji Mgeta alisema mahakama inao wajibu wa kupima kama maombi hayo ya Chadema yamekidhi vigezo vya kupewa kibali kufungua maombi hayo.

Moja ya kigezo kwa mujibu wa Jaji ni kwamba maombi ya aina hiyo yanatakiwa kufunguliwa ndani ya miezi sita tangu uamuzi unaolalamikiwa utolewe na maombi hayo yamefunguliwa ndani ya muda.

Kigezo cha pili ni kuwa waombaji ni lazima waonyeshe masilahi waliyonayo au imani waliyonayo kuwa wataathiriwa na uamuzi wowote utakaochukuliwa na Msajili na kigezo cha tatu ni uwepo wa shauri lenye msingi kuhusu suala hilo.

Jaji alisema baada ya kusikiliza pande mbili, anakubali kuwa Chadema wana masilahi au wanaamini wataathiriwa na uamuzi wa Msajili hivyo mahakama inaona wana kesi inayohitaji kuamuliwa na mahakama, hivyo wanaruhusiwa kufungua maombi ya mapitio.

Mbali na kutoa kibali cha kufungua maombi ya mapitio ya mahakama, Jaji alisema amri yake ya zuio la muda kwa Msajili wa vyama vya siasa, kuiadhibu Chadema linabaki pale pale hadi maombi hayo yatakapofunguliwa na kutolewa uamuzi na mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *