Dar es Salaam. Mradi wa ujenzi wa nyumba za Serikali unaotekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam umefikia asilimia 90 ya utekelezaji, huku ukitarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu na kuanza kupokea watumishi wa umma.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TBA, Laurean Ndumbaro, baada ya bodi hiyo kukamilisha kikao chake cha siku mbili kilichoambatana na ukaguzi wa miradi mbalimbali ya wakala huo jijini Dar es Salaam, ikiwemo mradi wa Magomeni Kota.

Ndumbaro amesema ameridhishwa na kasi na ubora wa ujenzi huo, akieleza kuwa mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali kupunguza upungufu wa nyumba za watumishi wa umma katika maeneo ya mijini.

“Tunatarajia ifikapo Oktoba mwaka huu mradi huu utakuwa umekamilika ili Watanzania, hususan watumishi wa umma wenye uhitaji wa makazi, waanze kunufaika na nyumba hizi,” amesema.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh11 bilioni unatekelezwa katika eneo la takribani hekta 32 za Magomeni Kota, mahali ambapo awali kulikuwa na nyumba 644 za zamani zilizokuwa zikikaliwa na wakazi kabla ya Serikali kuanza mpango wa kulifanyia maboresho eneo hilo.

Mkurugenzi wa idara ya miliki TBA, Said Mndeme amesema katika awamu ya sasa Serikali inajenga majengo matano ya kisasa yenye uwezo wa kuhudumia familia 80.

Tayari majengo mawili yenye uwezo wa kuhifadhi familia 32 yamekamilika na baadhi ya watumishi wa umma wameanza kuishi katika nyumba hizo.

“Majengo mengine mawili yenye uwezo wa kuhudumia familia 32 yako katika hatua za mwisho za ujenzi na yanatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026. Jengo la tano litakuwa na uwezo wa kuhudumia familia 16 na ujenzi wake unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu wa fedha,” amesema.

Mndeme amesema utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri na mara baada ya kukamilika kwa majengo hayo mawili yaliyosalia, watumishi wa umma wataanza kuhamia.

Mradi wa Magomeni Kota ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati ya TBA inayolenga kuongeza upatikanaji wa nyumba bora na za gharama nafuu kwa watumishi wa umma, huku ikiwezesha matumizi yenye tija ya ardhi ya Serikali.

Kukamilika kwa mradi huo kutachangia kuongeza upatikanaji wa makazi kwa watumishi wa umma na wananchi wengine wanaokidhi vigezo vya upangaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *