
Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria wa ACT Wazalendo, Peter Madeleka ametangaza kuachana na chama hicho, akisema anakwenda kuungana na wapenda haki.
Madeleka, aliyejiunga na ACT Wazalendo Mei 20, 2025 akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ametangaza uamuzi huo leo, Jumapili Julai 26, 2026.
Akiwa katika chama hicho, Mei 18, 2026, Madeleka aliteuliwa na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu, kuwa Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, wadhifa alioushika kwa mara ya pili tangu amejiunga ACT Wazalendo.
Katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Madeleka alikuwa mgombea ubunge wa Kivule ambapo alishindwa na mgombea wa CCM, Ojambi Massaburi.
Hata hivyo, chama hicho kimebariki uamuzi wake huo, kikisema ni haki yake ya kidemokrasia kuondoka au kujiunga na chama chochote cha siasa.
Taarifa ya kujiondoa
Katika ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani twitter), Madeleka ametangaza kuachana na siasa za ACT Wazalendo ili apate muda wa kutosha kuungana na wapenda haki.
“Nafanya hivyo ili nipate muda wa kutosha kuungana na wapenda haki wote katika kupigania haki na ustawi wa nchi yetu. Tanzania yenye haki inawezekana kama kila mtu atatimiza wajibu wake,” amesema.
Alipotafutwa kuthibitisha iwapo chapisho hilo ni lake, Madeleka amekiri la kwake, akisisitiza uamuzi huo umelenga kuungana na wapigania haki wengine nje ya chama alichokuwepo.
Amesema kwa kuwa yeye ni mwanasheria atatumia taaluma yake hiyo kuipigania haki kwani hilo ndilo jukwaa sahihi kwa haki.
“Kupigiania haki sio lazima kwenye jukwaa la kisiasa. Mimi ni wakili nitatumia tasnia ya sheria ambayo ni muhimu zaidi katika kupigania haki,” amesema.
Alipoulizwa ni chama gani anatarajia kujiunga nacho kupigania haki hiyo, Madeleka amesema ni mapema kuzungumzia hilo, akidokeza hayo ni mambo ya mbele hawezi kuyazungumza sasa.
Aidha, alipoulizwa iwapo ACT Wazalendo haipiganii haki ndio maana ameachana nayo, amesema hakusema hilo, lakini wananchi ndio wanajua zaidi.
“Nimeamua kuungana na wengine kupigania haki, suala kwamba ACT Wazalendo wanapigania haki au hawapiganii mimi sijasema na wananchi ndio wanaojua zaidi,” amesema.
ACT Wazalendo yabariki
Alipotafutwa na Mwananchi, kuzungumzia hilo, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita, amesema ni haki yake kidemokrasia kuamua kutoka chama kimoja kwenda kingine na wanamtakia kila la kheri.
Amesema Madeleka alijiunga na ACT Wazalendo kutoka Chadema, hivyo ana haki pia ya kutoka chama hicho kwenda kwingineko.
“Sisi tunaamini kwamba kama bado tutakuwa kwenye mapambano ya kupigania demokrasia na kutafuta suluhisho la matatizo ya Taifa letu tutakutana naye,” amesema Mchinjita.