Walowezi wa Kiisraeli wamevamia misikiti miwili, mmoja uliokuwa ukijengwa, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuichoma moto katika kile kinacholaaniwa kama kampeni ya kimfumo inayolenga haki za kidini za Wapalestina.

Shirika la habari la WAFA limeripoti kuwa mashambulizi hayo yalitokea mapema jana Jumapili dhidi ya msikiti wa kijiji cha Kur, katika Mkoa wa Tulkarm, na msikiti mwingine uliokuwa ukijengwa katika mji wa Qusra, katika Mkoa wa Nablus.

Walowezi wa Israel pia waliandika kauli mbiu za ubaguzi wa rangi kwenye kuta za misikiti hiyo iliyochomwa moto.

Abdel Azim Wadi, meya wa Qusra, amesema shambulizi dhidi ya msikiti wa mji huo limechoma vifaa vya mbao na zana za ujenzi.

Wakati huo huo, mashuhuda wa uhalifu huo wa walowezi wa Kizayuni huko Kur wamesema moto ulioteketeza sehemu za jengo la msikiti, ulizimwa na wakazi wa eneo hilo.

Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini wa Palestina imelaani mashambulizi hayo dhidi ya msikiti wa Kur ikiyataja kuwa ni “uhalifu mkubwa” unaolenga maeneo matakatifu ya Kiislamu. Imesema mashambulizi hayo yanakiuka kanuni na mikataba ya kimataifa inayohakikisha uhuru wa kuabudu na ulinzi wa maeneo matakatifu.

Imeongeza kuwa, mashambulizi dhidi ya misikiti yanayofanywa kwa usimamizi wa askari wa jeshi la Israel, yanazidi vitendo vya mtu binafsi na yanawakilisha kampeni ya kimfumo inayowalenga Wapalestina na haki za kidini.

Wizara hiyo pia imetoa wito kwa jamii ya kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuchukua hatua za haraka ili kukomesha mashambulizi kama hayo na kuwafikisha mbele ya sheria wale wanaohusika na uhalifu huo.

Wapalestina wa Ukingo wa Magharibi wanasumbuliwa na ongezeko la hujuma na mashambulizi ya jeshi la Israel na ukatili wa walowezi wa Kizayuni, huku vita vya mauaji ya kimbari vikiendelea katika Ukanda wa Gaza ambavyo vimeua zaidi ya watu 73,000 katika eneo hilo la pwani tangu Oktoba 2023.

Tangu wakati huo, jeshi la Israel na walowezi haramu wameua Wapalestina wasiopungua 1,182 kote Ukingo wa Magharibi, wakajeruhi maelfu, na kuwateka nyara wengine takriban 24,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *