.

Chanzo cha picha, IPN

Iliyochapishwa

Muda wa kusoma: Dakika 5

Tarehe 8 mwezi Januari mwaka wa 1996, Merced Guimarães dos Anjos, mama wa watoto watatu, alikuwa akitazama mafundi walipoanza kujenga sehemu ya nyumba yake iliyojengwa mwaka 1866.

Hii ilikuwa nyumba yake ya kwanza kuwahi kumiliki, katika eneo la bandari la Rio de Janeiro baada ya kuweka akiba ya kumiliki nyumba kwa muda wa miaka sita.

Lakini ndani ya saa chache, kazi hiyo ya ukarabati ilifichua jambo lisilotarajiwa, mifupa ya watu.

Mafundi walidhani mifupa hiyo ilikuwa ya wanyama, lakini Merced hakushawishika. Alianza kupekua vifusi na akagundua seti kamili ya meno ya mtu mzima.

“Nilimwambia fundi, ‘Hii si ya mbwa — ni ya binadamu,'” Merced aliiambia BBC News Brazil. “Mara moja fundi huyo alianza kujifanya ishara ya msalaba.”

Muda mfupi baadaye, Merced aligundua seti nyingine ndogo ya meno.

“Nilisema, haya ni ya mtoto. Kisha nikaanza kulia. Kila mtu aliganda kwa hofu.”

Picha ya Merced Guimarães dos Anjos

Chanzo cha picha, Júlia Dias Carneiro

Kadri mifupa zaidi ilivyozidi kupatikana mingi ikiwa vipande tu Merced alianza kuikusanya na kuipanga kwenye masanduku. Wakati huo huo, watu wakaanza kubashiri kuhusu kilichokuwa kimetokea.

“Mambo elfu moja yalipita akilini mwetu labda wamiliki wa awali waliwaua watu na kuwazika hapa, au labda kulikuwa na muuaji wa mfululizo.”

Lakini majibu yalipatikana haraka. Jirani mmoja, ambaye alifahamu historia ya eneo hilo, alifika akiwa na ramani ya zamani.

“Alinitazama na kusema, Unaishi juu ya makaburi. Hapa ndipo watu waliokuwa watumwa walizikwa.”

Bila kukusudia, Merced alikuwa amegundua Makaburi ya Pretos Novos, yaliyotumika takriban kati ya mwaka 1770 na 1830 na ambayo yalikuwa yamesahaulika kwa muda mrefu. Inakadiria kuwa watu 40,000 walizikwa hapo.

Wanahistoria walikuwa wakijua kwa muda mrefu kuhusu uwepo wa makaburi hayo kupitia kumbukumbu za makanisa, lakini eneo lake halisi lilikuwa limepotelea chini ya ardhi wakati jiji lilipokuwa likipanuka.

Neno “Pretos Novos” lilitumika kuwarejelea Waafrika waliokuwa wamefanywa watumwa na ambao walikuwa wamewasili nchini Brazil , wengi wao wakiwa bado hawajui kuzungumza Kireno.

.

Chanzo cha picha, IPN

“Tumekumbana na mauaji ya makubwa hapa, Holocaust ya watu weusi,” anasema Merced, akikumbuka mshtuko alioupata baada ya kugundua mifupa chini ya sakafu ya nyumba yake mwenyewe, ikiwemo mabaki ya watoto ambao meno yao yalikuwa bado hayajakua kikamilifu.

“Hatukujua kabisa. Hakuna mtu aliyewahi kutuambia kwamba hapa palikuwa mahali ambapo watu waliouzwa walizikwa. Sehemu hii ya historia ilifichwa.”

Karibu na hapo kulikuwa na Gati la Valongo, ambako meli zilizobeba watu waliokuwa wamefanywa watumwa zilitia nanga. Kuanzia mwishoni mwa karne ya 18 hadi lilipofungwa mwaka 1831, inakadiriwa kuwa Waafrika 900,000 walipitishwa kupitia gati hilo katika biashara ya utumwa, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Waafrika wengi zaidi waliokuwa wamefanywa watumwa walifika Rio de Janeiro kuliko jiji lolote jingine nchini Brazil.

Kwa kipindi cha zaidi ya karne tatu, inakadiriwa kuwa Waafrika milioni 4.8 waliletwa kwa nguvu nchini Brazil idadi kubwa kuliko nchi nyingine yoyote katika bara la Amerika kusini, kwa mujibu wa Trans-Atlantic Slave Trade Database ya Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.

Wengi walifariki kabla hata ya kufika ufukweni takriban watu 300,000, kwa mujibu wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Emory nchini Marekani.

Wengine walifariki kutokana na magonjwa au uchovu muda mfupi tu baada ya kuwasili, wakiwa katika maghala ambako walishikiliwa na kuuzwa. Wengi wa wale ambao walifariki walichukuliwa na kuzikwa katika makaburi ambayo sasa yako chini ya nyumba ya Merced.

Hazina ya kihistoria

Brazil pia ilikuwa nchi ya mwisho katika ulimwengu wa Magharibi kukomesha utumwa, mwaka wa 1888.

Hata hivyo, kwa miongo kadhaa, ni sehemu ndogo tu ya historia hiyo ya eneo hilo iliyotambuliwa hadharani. Katika miaka ya 1990, wakati Merced alipofanya ugunduzi huo, uhusiano wa eneo hilo na historia hiyo ulikuwa kwa kiasi kikubwa.

Hali ilianza kubadilika mwaka 2011, wakati Gati la Valongo lilipogunduliwa tena wakati wa kazi za uendelezaji wa eneo hilo kabla ya Michezo ya Olimpiki. Baadaye, eneo hilo lilitangazwa kuwa Tovuti ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, jambo lililosaidia kuangazia historia ya eneo hilo.

Merced alitambua kuwa alikuwa amegundua “hazina ya kihistoria” kwenye eneo lake, lakini hakujua afanye nini nayo.

Mwanzoni, alifungua nyumba yake kwa wageni mara chache tu, hasa wakati wa sikukuu kama Siku ya Uhamasishaji kuhusu Historia na Utamaduni wa Waafrika na Wamarekani na Siku ya Kukomeshwa kwa Utumwa.

“Ilikuwa vigumu,” anasema. “Nani angependa kutembelea makaburi?”

Lakini hamu ya watu kutembelea eneo hilo imeongezeka, pamoja na wito kutoka kwa wanaharakati wa kulindwa na kuhifadhiwa kwa eneo hilo.

.

Chanzo cha picha, IPN

Mwaka wa 2005, Merced na wengine walianzisha Taasisi ya Utafiti na Kumbukumbu ya Pretos Novos (IPN).

Eneo hilo limeendelea kubadilika taratibu. Eneo la kupakia gari imegeuzwa kuwa ukumbusho wenye maonesho ya kudumu. Sehemu ya nyuma ya nyumba ambayo awali ilikusudiwa kujengwa bwawa la kuogelea sasa ina mgahawa, duka dogo na maktaba yenye vitabu vinavyohusu biashara ya utumwa ya kuvuka Atlantiki na diaspora ya Waafrika.

Kioo kilichowekwa kwenye sakafu kinawawezesha wageni kutazama mabaki ya akiolojia yaliyo chini ya udongo wenye rangi nyekundu uliotapakaa vipande vingi visivyohesabika vya mifupa.

Kwa mujibu wa Merced, si sahihi kulielezea eneo hilo kama makaburi.

“Haya yalikuwa mashimo ambamo miili ilitupwa,” anasema. “Kwa sababu ya harufu, baadhi ya miili ilichomwa. Mashimo yalijaa kiasi kwamba miili ilibanwa na kukandamizwa juu ya nyingine.”

Kumbukumbu za kanisa zinathibitisha kuwa eneo hilo halikuwa la siri. Vifo vilirekodiwa rasmi, ingawa wengi wa waliokufa hawakutajwa majina walitambulishwa tu kwa tarehe, majina ya meli au maeneo walikotoka. Majina yanapoonekana kwenye kumbukumbu, mara nyingi huwa ni ya wamiliki wa watu waliokuwa wamefanywa watumwa.

“Makaburi haya yanaenea chini ya nyumba nne,” Merced anasema. “Kuna watoto wachanga, watoto, vijana, wanawake wajawazito watu kutoka Angola, Congo na Msumbiji.”

.

Chanzo cha picha, Divulgação

Sasa akiwa na umri wa miaka 69, Merced bado anaishi katika nyumba hiyo hiyo, karibu na eneo la kumbukumbu, na hufanya kazi hapo kila siku.

“Unapoondoa sakafu, unakuta mifupa mara moja chini ya ardhi,” anasema.

Takriban watu 300,000 wametembelea taasisi hiyo, huku wengine wengi zaidi wakitalii maeneo ya jirani, ambayo sasa yanajulikana kama Mzunguko wa Urithi wa Afrika

Kituo kipya cha utamaduni kilicho karibu kilizinduliwa kuadhimisha miaka 21 ya taasisi hiyo.

Merced anasema kituo hicho kitakuwa mwenyeji wa usomaji wa mashairi na mikutano,maonyesho ya sanaa, uzinduzi wa vitabu na vilabu vya usomaji kwa watoto, hasa wakati wa ziara za wanafunzi shuleni shughuli ambazo IPN tayari ilikuwa ikiandaa, lakini haikuwa na nafasi ya kutosha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *