
BAADA ya kuipandisha Kagera Sugar Ligi Kuu Bara, beki wa kati wa Yanga, Shaibu Mtita amerejeshwa kwenye kikosi cha Wananchi ili kuendelea kuipigania nafasi yake.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Yanga imeamua kumrudisha beki huyo baada ya kuridhishwa na maendeleo yake alipokuwa kwa mkopo katika Wakiso Giants na Kagera Sugar, huku ikionekana ipo tayari kumpa nafasi ya kuonyesha uwezo wake msimu wa 2026-2027.
Licha ya Wakiso Giants kuwa na msimu mbaya, beki huyo aliendelea kuaminiwa na benchi la ufundi, akicheza dakika 1,309 katika mechi 22 za Ligi Kuu ya Uganda akiwa beki tegemeo kwenye kikosi hicho.
Baada ya Wakiso kushuka daraja, beki huyo alijiunga na Kagera Sugar iliyokuwa inacheza Ligi ya Championship akaisaidia kupanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.
“Mbona yupo kambini anafanya mazoezi na timu ya wakubwa, wamemuongeza ili kuleta ushindani wa namba na kumtazama kwa karibu baada ya kupata muda mwingi wa kucheza ligi zenye ushindani,” alisema mmoja wa rafiki wa mchezaji huyo.
Mtita anarejea Yanga wakati ambapo kikosi hicho kina ushindani wa namba kwenye nafasi yake wapo Dickson Job, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Bakari Nondo na Mohamed Mussa aliyesajiliwa akitokea Mashujaa.
Mbali na Mtita ambaye anaonekana kupata uzoefu wa misimu miwili, Yanga pia imemrejesha kinda Hamis Nanguka aliyekuwa Mtibwa Sugar kwa mkopo.
Nanguka ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali kama beki wa kati, kulia na hata kiungo mkabaji kabla ya kutolewa kwa mkopo alikuwa anapata nafasi ya kucheza kwenye baadhi ya mechi.