
Kwa upande wa huku Bara, nilifahamika sana kwa jina la Masha. Kwa kule kwetu Zanzibar, jina lililozoeleka ni Zahrani. Ni mzaliwa wa kisiwa cha Pemba. Nilizaliwa Pemba. Nilisomea Pemba. Na huku Bara nilifika kwa ajili ya kazi tu.
Nilikuwa mfanyakazi wa gazeti la Kumekucha. Kazi yangu ilikuwa mwandishi wa habari.
Tangu nimekuwa katika gazeti hilo, nimepata umaarufu mkubwa katika sekta ya habari.
Niseme kwamba niliendelea kuipenda kazi yangu na kuithamini hadi siku hiyo ambayo sitaisahau, niliyotamani nife kuliko kuishi. Kulikuwa na msichana ambaye alikuwa akinipigia simu ofisini mara kwa mara, akiniambia kwamba alikuwa na habari muhimu ambayo alitaka kunipa. Aliniambia alikuwa akiishi Manzese na alinielekeza nifike nyumbani kwake Manzese.
Sikupenda kumpuuza. Niliona niende nikamsikilize. Kama atakuwa na habari ya maana kwangu, niifanyie kazi, na kama itakuwa ni habari ya kipuuzi, niachane naye.
Nilipofika kwenye kituo cha Manzese, nikashuka kwenye daladala, kisha nikatoa simu yangu na kumpigia.
Alipopokea simu, nikamwambia:
“Nimeshafika.”
“Uko wapi?” Sauti yake ikasikika kwenye simu.
“Niko hapa hapa kwenye kituo cha daladala.”
“Yaani umeshafika Manzese?”
“Ndiyo.”
“Asante sana. Ngoja nakufuata hapo hapo.”
“Usichelewe.”
“Sitachelewa. Hazitazidi dakika tano.”
“Sawa. Nakungoja.”
Nikakata simu na kusubiri hapo hapo.
Nilisubiri kwa muda wa kama dakika ishirini hivi, simu yangu ilipoita. Nilipotazama namba iliyokuwa inanipigia, nikaona namba ya yule msichana ambayo, ingawa sikuwa nimeihifadhi katika simu yangu, nilikuwa nimeikariri akilini mwangu.
“Hello…!” nikasema baada ya kuipokea simu.
“Unanisubiri wapi? Mimi nimeshafika.”
Nikatupa macho kila upande. Haikuwa rahisi kumtambua miongoni mwa watu waliokuwa wakipita mahali hapo.
“Upo kwa upande gani wa hiki kituo, kulia au kushoto?” nikamuuliza.
“Niko kushoto.”
Nikatupa macho upande wa kushoto. Hatua chache mbele yangu, nikamuona msichana amesimama huku ameweka simu sikioni akinitazama.
“Okey, hebu sogea karibu zaidi,” nikamwambia. Lengo langu lilikuwa kumtambua kama alikuwa ni yeye.
Nikamuona anasogea, nikajua ni yeye.
“Niko mbele yako,” nikamwambia.
Nikamuona anatabasamu na mimi nikatabasamu.
Alikuwa msichana mwenye weupe uliofifia. Alikuwa mrefu kiasi na mwenye mwili wa wastani.
Alikuwa amejifunga kitenge kilichouzunguka mwili wake.
Akakata simu na kuurudisha chini mkono uliokuwa umeshika simu. Ulikuwa mkono wa kulia. Akaipeleka simu kwenye mkono wake wa kushoto, kisha akanipa mkono wake wa kulia kunisalimia.
“Naitwa Sofia,” akaniambia.
“Na mimi naitwa Masha. Habari za muda huu?”
“Nzuri. Nashukuru kwa kukubali wito wangu, ingawa hatufahamiani. Sasa sijui twende nyumbani kwangu au sijui tutakwenda kuzungumzia wapi?”
“Nyumbani kwako ni mbali na hapa?” nikamuuliza.
“Si mbali. Tunaweza kwenda tu. Ni mtaa wa pili.”
“Okey, tunaweza kwenda.”
Tukaanza kutembea kwa miguu, tukikatiza kwenye vichochoro. Haukuwa mtaa wa pili kama alivyoniambia. Tulikwenda mbali zaidi. Kila mara nilikuwa natazama nyuma kuona kama nitaweza kurudi mwenyewe, kwani njia alizokuwa akinipitisha zilikuwa ni za vichochoro.
Hivyo vichochoro vilikuwa vikikatiza mbele ya nyumba za watu ambazo zilikuwa zimejengwa bila mpangilio. Tukatokea kwenye nyumba moja. Lilikuwa kama banda lisilo na mwelekeo maalum. Choo kilikuwa mbele ya nyumba pamoja na jiko.
Mlango wa banda hilo ulikuwa ni mmoja. Mbele ya banda palikuwa na mti wa mpera, na nilikuta wasichana watatu pamoja na watoto wadogo wasiopungua watano.
“Nyumbani kwangu ndiyo hapa,” msichana akaniambia.
Niliwasalimia wale wasichana. Mwenyeji wangu akaniambia:
“Karibu ndani.”
Yeye alikuwa ametangulia kuingia. Nikamfuata. Tulitokea kwenye ukumbi mwembamba ambao kila upande ulikuwa na vyumba viwili.
Msichana alikwenda kwenye mlango wa chumba cha pili upande wa kushoto. Akaufungua na kunikaribisha.
“Karibu.”
Tukaingia katika kile chumba. Kilikuwa chumba kidogo. Mbali na kitanda na kochi moja, vitu vingine vilikuwa vimerundikwa upande mmoja wa chumba, kama vile vilikuwa havijapangwa.
“Karibu ukae,” akaniambia.
Nikakaa kwenye lile kochi na yeye akakaa kwenye kitanda. Kulikuwa na redio ambayo ilikuwa ikipiga muziki, akaipunguza sauti.
“Hapa ndipo ninapoishi,” akaniambia tena, ingawa alishanitambulisha tangu tukiwa nje.
“Nimepafahamu,” nikamwambia, kisha nikatazama saa yangu na kujiweka sawa pale nilipokaa.
“Muda nao unazidi kuyoyoma. Ningependa unifahamishe kile ambacho ulitaka kunieleza.”
“Ni kuhusu mimi mwenyewe pamoja na aliyekuwa mume wangu.”
Nilikuwa nimeanza kukata tamaa aliponijibu hivyo. Nikamuuliza:
“Aliyekuwa mume wako ni nani?”
“Ni Joram Makita!”
Nikashituka kidogo kwa vile Makita alikuwa mtu mzito ambaye alijiuzulu wadhifa wa juu hivi karibuni.
“Joram Makita ndiye aliyekuwa mume wako?” nikamuuliza ili nipate uhakika.
“Ndiyo,” msichana akaniitikia kwa mkazo.
“Joram Makita huyu ambaye ni juzi juzi tu alijiuzulu wadhifa wake?”
“Ndiyo, yeye. Mpuuzi sana yule, amejiuzulu nini! Amefanya vile kwa akili yake.”
“Alikuwa ni mume wako wa ndoa kabisa?”
“Kwani sheria inasemaje, ukiishi na msichana kwa miezi sita tu ni mke wako na yeye ni mume wako? Yule nimeishi naye kwa miaka mitatu. Alikuwa amenipangia nyumba Mbezi.”
“Sasa nini kimetokea?”
“Nitakueleza. Kwanza nitaanza kukueleza mahusiano ya mimi na yeye. Yule bwana alinitongoza kwa ahadi ya kutaka kunioa, akanipangia nyumba Mbezi.”
“Nitakukatiza kidogo. Wakati akikutongoza wewe, hakuwa na mke mwingine?”
“Mke wake alishaachana naye.”
“Enhe… tuendelee…”
“Niliishi naye kama mke na mume hapo Mbezi, ingawa alikuwa na nyumba yake nyingine kule Masaki ambayo alikuwa akiishi na huyo mke wake aliyeachana naye.”
“Endelea…”
“Yule bwana alikuja kunipa mimba, akanishauri niitoe. Nikamuuliza kwa nini niitoe wakati mimi ni mke wake, akaniambia alikuwa hajanioa na, isitoshe, iliingia bila matarajio. Nikakataa kuitoa. Akanishawishi sana niitoe. Ili kunishawishi, alinipa shilingi milioni kumi. Nikakubali kwenda kuitoa…”
“Uliitolea wapi?”
“Kwa daktari mmoja ambaye alikuwa huku huku Manzese.”
“Baada ya kuitoa, nini kilitokea?”
“Kumbe alikuwa anataka kuniacha baada ya kupata mwanamke mwingine. Yule bwana, pamoja na heshima zake, ana tabia mbaya kwa wake zake. Sasa unapomkatalia, anakuacha na kutafuta mwanamke mwingine ambaye ataelewana naye.”
“Tabia hiyo ni ipi?”
“Ana tabia ya kwenda kinyume na maumbile.”
“Kwa hiyo alikuacha baada ya wewe kutokubaliana na hiyo tabia?”
“Ndiyo. Nadhani hata mke wake wa kwanza alimuacha kwa sababu hiyo hiyo.”
“Mhu… tuendelee.”
“Nilichogundua mimi ni kuwa yule bwana ni laghai na tapeli wa mapenzi. Ana tabia ya kubadilisha wasichana kama mashati. Kinachoniuma zaidi ni kuwa ameniacha mimi na kumchukua rafiki yangu Pete na Chanda. Na nina imani na yeye atamuacha, labda asikubaliane na tabia yake chafu. Kwanza, angalia umri wake ulinganishe na wasichana anaopenda kutembea nao, ni tofauti kabisa.”
“Ni kweli. Hata mimi nilikuwa nashangaa uliponiambia kwamba ulikuwa mke wake.”
Msichana huyo alitabasamu kidogo, ingawa sikujua ni kitu gani kilichomfanya atabasamu. Akaniuliza:
“Unajua ni kwa nini yule bwana alijiuzulu wadhifa wake?”
“Sijui ni kwa nini.”
“Nitakwambia kwa sababu aliwahi kunieleza siri zake nyingi.”
“Hizo ndizo ninazozitaka mimi.”
“Amejiuzulu kwa sababu amepata hofu, akijiona kuwa mtumishi wa serikali huku akiwa amemiliki mali nyingi ambazo asingeweza kuzitolea maelezo. Yule bwana ana nyumba sitini hapa nchini na ana hoteli nne kubwa. Hata kama angefanya kazi serikalini kwa miaka mia moja, asingeweza kuwa na mali kama hizo.”
“Hizo nyumba sitini ziko wapi?”
“Hapa Dar peke yake ana nyumba arobaini. Masaki ana nyumba saba, Mbezi ana nyumba kumi, Kigamboni ana nyumba sita. Nyumba nyingine ziko Oysterbay na Msasani. Dodoma ana nyumba nne. Huko kwao Mwanza ana nyumba ishirini. Hizi nyumba zote amezipangisha. Mapato ya nyumba hizo kwa mwaka ni mamilioni ya pesa anayoingiza yule baba.”
“Wewe una ushahidi gani kuwa hizo nyumba ulizotaja ni zake?”
“Aliwahi kuniambia mwenyewe na aliwahi kunionesha baadhi ya hati za nyumba hizo zikiwa na jina lake.”
“Na hizo hoteli ulizosema ni zipi?”
“Moja ni New Star. Ipo Masaki. Nyingine pia inaitwa hivyo hivyo, ipo Kibaha. Mwanza anazo hoteli mbili. Hizo hoteli zote nilishafika na nilishalala.”