
Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, Ahmad Donyamali amewataka mawaziri wenzake katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuunda muungano wa pamoja dhidi ya utawala wa Israel ambao utasaidia kuupiga marufuku utawala huo wa Kizayuni kwenye michezo ya kimataifa.
Katika barua kwa mawaziri wa michezo wa nchi 57 wanachama wa OIC, Donyamali amesema kuna haja ya kuunda “Mrengo wa Umoja wa Kiislamu Michezo” (Unified Islamic Sports Front) ili kuitaka Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kusimamisha uwepo wa utawala wa Israel katika michezo ya kimataifa.
Amesema katika barua hiyo kwamba, utawala ghasibu wa Israel umehujumu pakubwa Mkataba wa Olimpiki na moyo wa kweli wa michezo kupitia hatua zake dhidi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu katika kipindi cha miongo minane iliyopita, na hasa tangu Oktoba 2023, ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wananchi wa Palestina huko Gaza.
Mkataba wa Kimataifa wa Kupinga Ubaguzi wa Rangi katika Michezo (uliopasishwa na Umoja wa Mataifa mwaka wa 1985) unathibitisha wazi kwamba, michezo haipaswi kuwa jukwaa la kuhalalisha tawala zilizoanzishwa kupitia ubaguzi na ukandamizaji.
Donyamali amesema nchi wanachama wa OIC zinapaswa kutaka rasmi kusimamishwa na kufukuzwa Israel katika mashindano ya kimataifa ya michezo.
Hivi karibuni pia, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilitoa wito wa kutimuliwa Israel katika soka kutokana na mauaji yake ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Amir Mehdi Alavi, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Shirikisho la Kandanda la Iran alibainisha kuwa, Shirikisho la Soka la Iran limetuma barua mara kadhaa kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka la Asia (AFC) likitaka kusimamishwa uanachama wa shirikisho la soka la utawala wa kizayuni wa Israel kutokana utawala huo ghasibu kutekeleza mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Palestina, zaidi ya wanamichezo 800 wameuawa shahidi tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha hujuma na mashambulio ya kinyama dhidi ya Gaza Oktoba 2023.