Bunge la Chad limeidhinisha kwa wingi mkubwa sana wa kura marekebisho ya katiba yanayoondoa ukomo wa mihula ya urais, na kurefusha muda wa kila muhula kutoka miaka mitano hadi saba, hatua ambayo wakosoaji wanasema ni mbinu ya kuuzatiti utawala wa Rais Mahamat Idriss Deby Itno.

Uamuzi huo wenye utata, unafungua njia kwa Deby kuweza kusalia madarakani kwa miongo kadhaa.

Marekebisho hayo, yaliyowasilishw na Chama cha rais Deby cha Patriotic Salvation Movement (MPS), yameidhinishwa na wabunge 236 kati ya 257.

Kura hiyo ilisusiwa na baadhi ya wabunge wa upinzani, huku wabunge wa chama cha Mkutano wa Kitaifa wa Wanademokrasia wa Chad wakiamua kutoka nje ya ukumbi wa bunge wakati wa upigaji kura.

Kiongozi wa upinzani Albert Pahimi Padacke amelaani mabadiliko hayo na kusema ni “kinyume cha katiba na yamefanywa kimabavu,” msimamo unaoashiria mpasuko wa kisiasa unaozidi kuongezeka nchini Chad.

Mabadiliko hayo yanaongeza pia mihula ya bunge na kurejesha kinga kwa maafisa wa serikali.

Marekebisho hayo ya katiba yanaimarisha mamlaka ya Deby, ambaye alichukua nafasi ya kiongozi wa mpito mnamo mwaka 2021 baada ya kifo cha babake na akashinda uchaguzi uliolalamikiwa uliofanyika Mei 2024…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *