
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa, waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu ndiye aliyetoa idhini ya kufanywa mashambulio ya ndege zisizo na rubani yaliyolenga msafara wa kimataifa wa meli za misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Ghaza zilizokuwa zimetia nanga kwenye bandari ya Tunisia.
Shirika la utangazaji la CBS la nchini Marekani limewanukuu maafisa kadhaa wa intelijensia wa nchi hiyo ambao wamethibitisha kwamba mashambulio ya tarehe 8 na 9 za mwezi uliopita wa Septemba dhidi ya meli za msafara wa kimataifa wa Sumud chini Tunisia yalifanywa kutokea kwenye nyambizi ya jeshi la utawala wa kizayuni wa Israel.
Ripoti hiyo ya CBS imetupilia mbali rai za wachambuzi wanaoiunga mkono Israel kwamba moto uliotokea kwenye meli hizo ulitokana na utumiaji usio sahahi wa bunduki za moto unaofyatuliwa angani za wanaharakati waliokuwemo kwenye meli hizo.
Katika taarifa uliyotoa siku ya Ijumaa, masafara huo wa meli za misaada ulisema unaushuku utawala wa Israel kuwa ndio uliohusika na mashambulio hayo, ambayo hayakusababisha maafa ya roho za watu.
“Kuthibitishwa kwamba Israel ilihusika hakujatushangaza…ilieleza taarifa ya Sumud na kuongezea kwa kusema: “liwe lengo la mashambulizi haya ya kiholela ni kutuua, kututisha au kuziharibu boti zetu, yalifanywa bila kujali kwamba yanahatarisha raia na watu waliojitolea kutoa misaada ya kibinadamu. Ulimwengu lazima uzingatie: majaribio ya kunyamazisha, kutisha au kuzuia dhamira yetu kwa piganio la Palestina na watu wake hayatafanikiwa. Tunatoa wito wa kufanyika uchunguzi huru na wa haraka kuhusu mashambulizi haya na kuwajibishwa kikamilifu waliohusika”…/