
Wakati wapiga kura wakitumia majukwaa ya mitandaoni kuonesha ukubwa wa kampeni zao na kuwanadi wagombea wao, wananchi wanaoelemea upande wa vyama vilivyoamua kutoshiriki uchaguzi huu wanatumia uwanja huo wa kidijitali kuonesha hali inayopamba moto wakitiana hamasa juu ya kile kitakachotokea hapo Oktoba 29.
Lakini wakati taarifa sahihi zikisaidia katika maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, taarifa potofu, maudhui ya kughushi, na propaganda zenye malengo maalum nazo zimekuwa zikienea kwa kasi katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Mchango wa mitandao ya kijamii
Wadau wa habari, asasi za kiraia, wanasiasa na wananchi wenyewe wameonya kuhusu kusambaa kwa taarifa potofu kupitia majukwaa ya kidijitali ambao unaweza kuathiri matokeo ya uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani.
Taarifa potofu pia zinaathiri uchumi na biashara za mataifa, Tanzania ikiwemo. Kwa mujibu wa Ripoti ya Jukwaa la Uchumi Duniani (World Economic Forum) maudhui potofu yametajwa kuwa tishio kuu kwa mwaka 2025 kwa pato la dunia (GDP), watu, rasilimali za asili kuliko hata mabadiliko ya tabianchi na migogoro ya kivita.
Athari kwa vyama vya siasa
Vyama vya siasa ambavyo vimekumbana na kadhia hii ya taarifa potofu, vimewahi kufanya jitihada kupambana na changamoto hiyo. Mnamo Julai mwaka huu, Chama cha Mapinduzi, CCM kilitambulisha matumizi ya nambari maalum, ama QR Code ili kuwasaidia wananchi kuhakiki taarifa rasmi zinazotolewa na chama hicho.
Utafiti uliofanywa na Taasisi ya masuala ya kidijitali ya Jamii Check, kati ya Januari na Juni 2025 kuhusu taarifa potofu umebaini kuwa katika kipindi hicho, taarifa za uongo zilizobainishwa ni 128 sawa na asilimia 67 wakati taarifa za uongo kuhusu masuala ya uchaguzi zilikuwa 121 sawa na asilimia 63.
Miongoni mwa taarifa potofu ni pamoja na ile iliyosambazwa mitandaoni ikisema Chadema yaitupilia mbali kampeni yake ya No Election 29, ambayo inahamasisha wananchi kutoshiriki uchaguzi wa Oktoba 29.