Dar es Salaam. Serikali imebainisha kuwa mageuzi yanayoendelea katika sekta ya Posta ni sehemu muhimu ya kukuza uchumi wa kidijitali na kuimarisha huduma za mawasiliano na biashara nchini.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 9, 2025.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkapa amesema kaulimbiu ya mwaka huu: “Posta kwa ajili ya watu: Huduma za Kizawa, Ufikaji Kimataifa”, inalenga kuifanya sekta ya posta kuwa injini ya maendeleo endelevu kupitia matumizi ya Tehama, ubunifu na ujumuishi wa wadau wote.
Amesema sekta hiyo imebadilika kutoka mfumo wa jadi wa barua hadi kuwa mhimili wa biashara mtandao na usafirishaji wa bidhaa, jambo linalowawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Mkapa amesema mageuzi hayo yameiwezesha posta kutoa huduma bora zaidi, kupunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa, na kufungua fursa za ajira na ubunifu.
“Nawataka watoa huduma wa posta wa umma na binafsi kuendelea kubuni mifumo ya kisasa itakayowezesha huduma kufika maeneo yote nchini, ikiwemo vijijini, ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayebaki nyuma katika mapinduzi ya kidijitali,” amesema.
Katika tukio hilo, Katibu Mkuu huyo amekabidhi zawadi kwa washindi wa Shindano la Uandishi wa Barua Kimataifa na Shindano la Ubunifu wa Mifumo ya Posta.
Amesema mashindano hayo ni sehemu ya kukuza vipaji na kuwajengea vijana uwezo wa kufikiri kimkakati, kuandika kwa ubunifu na kutumia teknolojia katika kutatua changamoto za kijamii.
“Serikali inatambua nafasi ya vijana katika mageuzi ya kidijitali, mashindano ya ubunifu yanayoratibiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni fursa muhimu ya kuibua mawazo mapya yatakayochochea maendeleo ya sekta mbalimbali nchini,” amesema.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Posta na Vifurushi kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Caroline Kanuti amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma wa posta, wa umma na binafsi.
Amesema lengo ni kuhakikisha huduma bora na za kisasa zinawafikia wananchi katika maeneo yote nchini, ikiwa ni pamoja na vijijini.
Kwa upande wake, Kaimu Posta Masta Mkuu Shirika la Posta Tanzania, Arubee Ngaluka amesema mashindano ya ubunifu wa mifumo ya posta na uandishi wa barua kimataifa ni sehemu ya kukuza vipaji, kuongeza ubunifu na kuandaa vijana kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.