DILI la kocha Romuald Rakotondrabe ‘Roro’ ndani ya Yanga limeingia utata ambao unatishia hata ujio wake kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara.

Iko hivi, Roro alishamaliza makubaliano katika mambo mengi na Yanga, hilo sio shida, lakini utata ambao umeibuka ni namna ya muundo wa benchi lake la ufundi kwani hapo ndipo umeibuka mjadala.

Roro anataka kutua Yanga akiwa na watu wawili ambapo wa kwanza ni mmoja wa wasaidizi wake namba moja, lakini changamoto ambayo imeibuka ni msaidizi huyo kuwa na leseni ambayo haikidhi matakwa ya kuwa kocha msaidizi, huku Roro mwenyewe akisisitiza kwamba huyo ndiye mtu anayemwamini na anataka atue naye nchini.

Lakini, duru kutoka ndani ya Yanga zinadai kwamba imemshauri kocha huyo kama hana mtu muafaka anayekidhi vigezo basi imsaidie kutafuta makocha watatu kisha yeye amchague mmoja.

Hesabu za Yanga pia ni kwamba inalenga kumtafutia kocha huyo msaidizi ambaye atamsaidia kwenye lugha ya kuwasiliana na wachezaji kwani Roro anajua kuzungumza kwa ufasaha Kifaransa tu.

“Hatuna shida hata akimleta msaidizi wake kama anataka kwa kuwa huyo anakuja kufanya naye kazi yeye sio sisi. Shida mtu anayemtaka hakidhi vigezo na hatutaki kuwa kama timu nyingine za kuwa na watu wasiokuwa na vigezo,” amesema kiongozi mmoja kutoka ndani ya Yanga kwa sharti la jina lake kutotajwa.

“Hili la wasaidizi kisha achague ni katika kumsaidia tu ili kuondokana na huo wakati mgumu aliokutana nao hasa baada ya kutuambia yule ambaye alikuwa naye kwenye CHAN hawezi kuja naye.”

Utata wa pili kuhusiana na dili la kocha huyo ni ishu ya kocha wa mazoezi ya viungo, ambapo Roro anataka kuja na kocha wake, lakini viongozi wa Yanga wameridhishwa sana na yule wa sasa Tshephang ‘Chyna’ Mokaila ambaye ni raia wa Botswana.

Mokaila alitua mapema wakati Yanga inaunda benchi la kocha Romain Folz, lakini namna anavyowapigisha mazoezi wachezaji ni kwamba kila bosi amegoma jamaa kuondoka.

“Tunamuondoa Folz kwa kuwa hatukubaliani sana na namna timu inavyocheza, lakini sidhani kama kuna mtu hata kwa mashabiki anaweza kusema wachezaji wetu hawapo fiti. Huyu Mokaila amefanya kazi vizuri sana,” amesema kiongozi huyo.

“Tumezungumza naye na amekubali kubaki na sisi tunataka abaki. Tumemshauri kocha (Roro) lakini ni kama anataka kung’ang’ania kuja na msaidizi wake…ukweli kuna ugumu hapo.

ROR 01

“Bado hatuwezi kusema moja kwa moja kwamba hataweza kuja, lakini kuna huo utata lazima kila upande utafute suluhu.” 

Aliongeza kuwa: “Bado tuna kocha (Folz) kwa hiyo kama tutapata muafaka mambo yataendelea.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *