
Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini imempa jukumu Cedrick Kaze kuinoa timu hiyo hadi mwishoni mwa msimu kufuatia uamuzi wa kuachana na Kocha wake Mkuu, Nasreddine Nabi jana.
Kaze kabla ya kubebeshwa jukumu hilo la kukaimu nafasi ya Ukocha Mkuu, alikuwa kocha msaidizi katika kikosi hicho, nafasi ambayo aliipata kutokana na kupendekezwa na Nabi.
Taarifa iliyotolewa na Kaizer Chiefs imefafanua kwamba Kaze ataiongoza timu hiyo kwa kushirikiana na Khalil Ben Youssef.
“Kufuatia taarifa ya kuachana kwa makubaliano baina ya Kaizer Chiefs FC na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, klabu inathibitisha kwamba makocha Khalil Ben Youssef na Cedric Kaze, wataongoza benchi la ufundi kwa kipindi chote kilichobakia cha msimu.
“Usimamizi wao utahakikisha muendelezo na uimara wakati klabu ikiendelea kujiandaa na mechi zijazo za ndani na ya bara,” imesema taarifa ya Kaizer Chiefs.
Kwa upande wake Nabi, ameishukuru Kaizer Chiefs kwa fursa iliyompa ya kuinoa huku akiwasihi wachezaji kupambania nembo ya klabu hiyo.
“Kwa wachezaji wangu, nitashindwa kuwaambia kwaheri na kuwakumbatia kama nilivyotamani lakini mjue kwamba nina fahari kwa ajili yenu na nawashukuru kwa juhudi zenu mlizofanya katika kipindi changu klabuni.
“Kwa wachezaji wenye umri mdogo, nyie ni vito vya thamani kwa klabu. Jiaminini, fanyeni kazi na mjifunze katika kila nyakati. Nawasihi muwe na ndoto kubwa kwa vipawa vyenu na muwe na matarajio makubwa yaliyo sawa na vipaji vyenu,” amesema Nabi.
Nabi ameondoka Kaizer Chiefs akiwa ameipa timu hiyo taji moja ambalo ni Nedbank walilolitwaa msimu uliopita.